Habari

Imewekwa: Feb, 11 2024

​Waziri Mkuu awataka wadau wa sekta ya maji kushirikiana katika utunzaji wa vyanzo vya maji.

News Images

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amezitaka Taasisi za Umma, sekta binafsi na wadau wa sekta ya maji kuhakikisha wanachukua hatua za haraka za kuhakikisha vyazo vya maji vinalindwa na kuendelezwa.

Maagizo hayo ameyatoa wakati akifungua Mkutano wa sita wa Jukwaa la Kitaifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema maji ni rasilimali muhimu ambayo inahitaji ushiriki kwa kila mdau katika ulinzi kwa ajili ya vizazi vya sasa na baadaye.

Mhe. Waziri Mkuu Majaliwa katika agizo la kwanza amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinachukua hatua za haraka za kuzuia shughuli zinazohatarisha uhai wa vyanzo vya maji. Amesema waharibifu wa vyanzo vya maji wako katika jamii ambayo iko chini ya viongozi wa halmashauri.

Viongozi wa halmashauri wachukue hatua za haraka kuzuia viashiria vya uharibifu ikiwemo ongezeko la mifugo, wakulima wasiozingatia sheria, wachimbaji wa madini, na makundi mengine yanayohatarisha uhai wa vyanzo vya maji.

Pamoja na hayo, amezitaka halmashauri kuongeza kasi katika uwekezaji wa miundombinu ya kuvuna maji ikiwemo ujenzi wa mabwawa na kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua kupitia majengo ya nyumba za wananchi na taasisi.

Ameitaka Wizara ya Maji kuhakikisha Bodi za Maji za Mabonde zinaongeza jitihada katika kutambua na kutangaza vyanzo vya maji ili vilindwe kwa mujibu wa sheria.

Maelekezo haya yamezigusa sekta binafsi na taasisi nyingine za serikali kuhakikisha zinatenga fedha kwa ajili mipango ya uendelezaji wa rasilimali za maji. Wizara ya Madini idhibiti uchimbaji wa madini usiozingatia sheria, na kuepuka kutoa vibali katika maeneo yasiyo ruhusiwa.

Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kutumia majukwaa ya ibada kufikisha ujumbe wa utunzaji wa vyanzo vya maji kwa wananchi.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema wizara imeendelea na jitihada mbalimbali ikiwemo kuhakikisha jamii nzima inashiriki kutunza na kulinda vyanzo vya maji. Aidha kuendelea na uhuishaji wa sera ya maji ili iendane na mahitaji ya sasa na kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta ya maji.

Pia, sheria na Muundo wa Bodi za Maji za Mabonde umefanyiwa maboresho ili kutatua changamoto nyingi ambazo wamekuwa wakikutana nazo.

Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) amewataka wadau wote wa jukwaa kutoa ushirikiano kwa wizara kutokana na hatua mbalimbali wanazochukua kukabiliana na changamoto za uharibifu wa vyanzo vya maji. Amewakumbusha wajumbe kuhusu utabiri wa wataalam na viongozi mbalimbali kwamba hatua zisipochukuliwa kwa haraka, migogoro katika jamii itasababishwa na changamoto za uhaba wa maji.

Mkutano wa sita wa Jukwaa la Kitaifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini mwaka 2024 umebeba kaulimbiu isemayo; Majanga ya Mafuriko na Ukame: Uwekezaji katika Usalama wa Maji ni Jambo la Haraka (Floods and Droughts Disasters: Investment in Water Security is an urgent issue)”.