Habari

Imewekwa: May, 03 2021

Watumishi wa Wizara ya Maji waaswa kuzingatia Sheria

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka watumishi wa Wizara ya Maji kote nchini kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma ili kuleta tija katika utendaji kazi. Wito huo ameutoa leo Mei 3, 2021 mjini Dodoma wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo.

Amesema Vyama na Mabaraza ya wafanyakazi yameundwa kwa sababu za msingi za kuhakikisha kunakuwepo na ufanisi katika utendaji kazi. Bila kufanya hivyo Vyama au Mabaraza ya wafanyakazi yatakuwa yanachochea migogro na malalamiko katika sehemu ya kazi.

“Mahali ambapo Chama au Baraza la Wafanyakazi, kazi yake kubwa ni kushughulikia tu kero za watumishi bila kusimamia viwango vya uzalishaji au ufanisi wa kazi, pataendelea kuwa na migogooro isiyoisha ya watumishi wanaodai maslahi bila kutimiza wajibu.” Aweso amesema.

Amesisitiza kuwa Wizara ya Maji itahakikisha inatoa ushirikiano kwa Vyama na Mabaraza ya Wafanyakazi kwani kufanya hivyo kunasaidia kuwa karibu na wadau wa sekta ya Maji na hivyo kurahisisha suala zima la upatikanaji wa majisafi, salama na yenye kutosheleza kwa wananchi.