Habari

Imewekwa: Dec, 17 2021

Wadau wa Sekta ya Maji Wakutana Kutatua Changamoto ya Upungufu wa Chanzo cha Mto Ruvu

News Images

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau wote katika jitihada za kusimamia, kutunza na kulinda vyanzo vya maji ili kufikia lengo la kuwa na vyanzo vya maji toshelevu kwa maendelo ya taifa kwa miaka mingi ijayo.

Mhandisi Kemikimba ametoa rai hiyo wakati akifungua Jukwaa la Wadau lililokuwa likijadili Kulinda Rasilimali za Maji katika Bonde la Wami-Ruvu kwa dhumuni la kupata suluhisho la kudumu la uhakika wa maji katika chanzo cha Mto Ruvu kwa ajili ya mkoa wa Dar es Salaam lililofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Kemikimba amesema dhana ya ushirikishwaji kwa wadau wote muhimu kwa lengo la kuwa na uelewa na jitihada za pamoja katika kufanikisha uendelevu wa vyanzo vya maji nchini, akitolea mfano umuhimu wa mikakati madhubuti ya kulinda na kutunza Mto Ruvu kwa mustakbali wa mkoa wa Dar es Salaam na vitongoji vyake kuwa na maji ya uhakika ikizingatiwa kuwa ni kitovu cha biashara kwa nchi ya Tanzania.

Akisema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa maji yanakuwepo ya kutosha kwa matumizi yote, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika kutatua changamoto zote zinazotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu kwa kukaa pamoja na wadau wote.

Awali, Kaimu Afisa Maji wa Bodi ya Maji ya Bonde, Mhandisi Elibariki Mmasi amesema ushirikishwaji wa jamii katika kulinda, kutunza na kuendeleza rasilimaji za maji ni lazima ma kusisitiza kuwa lengo la jukwaa hilo ni litatoka na mipango, mikakati na suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta ya maji kwenye Mto Ruvu ikiwemo kuhifadhi maji kwa njia mbadala kwa ajili ya matumizi kipindi cha ukame ili changamoto ya upungufu wa maji kwa mkoa wa Dar es Salaam isijirudie tena kwa siku za usoni.

Jukwaa lililoandaliwa na Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu na kufadhiliwa na UNDP limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka Wizara ya Maji, wizara mtambuka, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira.