Habari

Imewekwa: Jun, 06 2023

​Ushirikishwaji wadau Sekta ya Maji wawaleta UKEF wa Uingereza

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la UK Export Finance (UKEF), Bwn. Tim Reid kuhusu Sekta ya Maji na maendeleo yake hapa nchini.

Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dodoma ambapo ni matokeo ya ziara ya Mhe. Aweso aliyoifanya hivi karibuni nchini Uingereza na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa lengo la kushirikiana katika utatuzi wa changamoto zinazoikumba Sekta ya Maji nchini Tanzania.

Waziri Aweso katika mazungumzo hayo amemhakikishia Bwn. Reid kuwa serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana na UKEF katika kuhakikisha malengo yake yanafikiwa.

Amesema Wizara ya Maji ipo katika mipango mbalimbali mahsusi yenye lengo la kuhakikiha mama wa Tanzania anatua ndoo ya maji kichwani na jitihada hizo haziwezi kufanikiwa bila ushirikishwaji na kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo UKEF.

Kwa upande wake Bwn, Reid amemhakikishia Waziri Aweso kuwa UKEF iko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kutokana na utayari ambao ameuonesha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na timu yake wakiwamo viongozi wa Wizara ya Maji katika kujenga ushirikiano na mataifa ya nje ikiwamo nchi ya Uingereza.

Amemuomba Waziri Aweso afikishe salam zake kwa Mhe. Rais kuwa UKEF wana imani kubwa na serikali anayoiongoza hivyo wako tayari wakati wowote kuendeleza ushirikiano huo kwa kupitia Sekta ya Maji.

Pamoja na Mhe. Aweso, katika kikao kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba pamoja na wataalam wa Wizara ya Maji.