Habari
Tanzania, Msumbiji na Malawi wasaini makubaliano ya ushirikiano Bonde la Mto Ruvuma
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) pamoja na Mawaziri wenza wanaosimamia sekta ya maji kutoka nchi za Malawi na Msumbiji wamesaini makubaliano yenye lengo la kuweka mikakati ya pamoja katika utunzaji, ulinzi na uendelezaji wa Bonde la Mto Ruvuma.
Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Dar es Salaam ambapo upande wa Malawi wamewakilishwa na Waziri wa Maji Mhe. Abida Sidik Mia na nchi ya Msumbiji ikiwakilishwa na Waziri wa Maji Mhe. Carlos Mesquita.
Katika mkutano huo Waziri Aweso amesema suala la usimamizi wa rasilimali maji lazima liwe la pamoja ili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa yakiathiri rasilimali hiyo kwa muda mrefu. Amesema ndoto ya waasisi wa Serikali zote tatu ilikuwa ni kudumisha umoja kizazi hadi kizazi.
“Hayati Mwalimu Nyerere alisema bila umoja hakuna maendeleo Afrika, Hayati Samora Machel wa Msumbiji akasema ili taifa liendelee kuwa salama lazima ukabila uondoke (For the Nation to live, the tribe must die). Aidha hata nembo ya taifa la Malawi inaelezea Umoja na Uhuru. Mhe. Aweso ameongeza
Aidha, Waziri Aweso amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo, taasisi na sekta zote kujitokeza ili kusaidia jitihada hizo zilizoanzishwa huku akisisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yuko tayari kuhakikisha ushirikiano huo unaendelelea kuimarishwa.
Kwa upande wa Waziri Sidik Mia kutoka Malawi amesema mafanikio ya usalama wa bonde la Mto Ruvuma ni heshima kwao na vizazi vijavyo hivyo lazima wote kwa pamoja wahakikishe kazi hiyo inafanikiwa, huku Mhe. Carlos Mosquita wa Msumbiji akisisitiza umoja na kuwataka Wanachi na wadau wote kutoa ushirikiano.