Habari

Imewekwa: Jun, 05 2024

​Naibu Waziri maji apokea taarifa ya wataalamu kuhusu dira za maji za malipo Kabla.

News Images

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew (Mb) amepokea taarifa ya awali ya wataalam wa wizara iliyoundwa kwa ajili ya kufanya utafiti wa `namna bora ya kuingia rasmi katika matumizi ya dira za malipo kabla. Kabla ya taarifa hiyo Mhe. Mathew amepokea mawasilisho kutoka kampuni zinazotengeneza na kusambaza dira za malipo kabla sehemu mbalimbali duniani ambazo zinalenga kutoa huduma hiyo hapa nchini.

Mhe. Mathew amesema matumizi ya dira mpya za malipo kabla ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye anapambana kuhakikisha changamoto zote zinakwamisha utoaji huduma ya maji kwa Watanzania zinapatiwa ufumbuzi. Aidha, Wizara inafanya kila linalowezekana ili uekelezaji huo ufanyike mara moja kwa viwango sahihi.

Amesema Wizara imekuwa ikitoa huduma hiyo katika sehemu mbalimbali nchini ambapo changamoto mbalimbali zimekuwa zikijitokeza jambo ambalo limefanya wizara ione umuhimu wa kufanya utafiti wa kina ambao utafanya maamuzi ya kupata teknolojia na mkandarasi bora ambaye ataweza kuondoa changomoto zote ambazo zimekuwa zikijitokeza.

Pia itawezesha taasisi zote za serikali ambazo zinatoa huduma ya maji kuwa na mfumo wa aina moja ambao utawezesha ushirikiano wa teknolojia na utatuzi wa changamoto.

Mhe. Mathew ameipa timu hiyo siku 14 za kuwasilisha taarifa ya kina ambayo itafanya maamuzi na kuanza utekelezaji wa pamoja unaofanana kwa kila mtoa huduma.