Habari

Imewekwa: Aug, 15 2019

Kazi ya Ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mugango - Kiabakari - Butiama: Kuanza

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Mkataba wa kuanza utekelezaji wa mradi wa maji wa Mugango – Kiabakari – Butiama umesainiwa leo katika viwanja vya shule ya msingi Nyamisisye (Kiabakari) na kushuhudiwa na viongozi pamoja na wakazi wa mkoa wa Mara.

Mkataba huo umesainiwa baina ya serikali na kampuni za Metito (Overseas) kutoka Misri na kampuni ya Jandu Plambers ya nchini.

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Prof. Kitila Mkumbo akiongea katika hafla hiyo amesema serikali imeamua kutumia ziwa Viktoria kama chanzo cha maji kwa miradi ya maji itakayotekelezwa maeneo kanda ya ziwa. Aidha, amesisitiza utaalam utazingatiwa ili kuepuka matatizo kwa watumiaji wengine wanaotegemea ziwa hilo.

Prof. Kitila amesema hadi itakapofika mwanzoni mwa mwaka kesho 2020 serikali itakua imetumia kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kwa uwekezaji wa miradi ya maji ya kuhudumia wananchi katika maeneo mbalimbali ya kanda ya ziwa.

Ameongeza kuwa miradi hiyo inayotekelezwa ni ya wananchi hivyo kila mmoja kwa nafasi yake afuatilie maendeleo yake, na endapo kuna tatizo taarifa itolewa bila kusita ili hatua zichukuliwe mara moja.

Prof. Kitila ameongeza kuwa uwekezaji wa serikali katika miradi ya maji umeongeza hali ya upatikanaji maji nchini hadi kufikia asilimia 71, ambapo takwimu zinaonyesha toka awamu ya tano iingie madarakani kwa vijijini hali ya upatikanaji maji imepanda kutoka asilimia 46 mwaka 2015 hadi asilimia 64 mwaka 2019, na mijini kwa kipindi hicho imetoka asilimia 74 hadi asilimia 84.

Mradi wa maji wa Mugango – Kiabakari – Butiamaunatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24 na utaongeza hali ya upatikanaji maji katika maeneo hayo kutoka asilimia 67 ya sasa hadi kufikia asilimia 100. Mradi huu unatekelezwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ambao ni Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA), na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (SFD).

Kitengo cha Mawasiliano

15 Agosti, 2019