Habari

Imewekwa: Jun, 02 2023

Mhandisi Mahundi aitaka Bodi ya DUWASA kuweka mikakati kupunguza upotevu wa maji

News Images

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ameitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kushirikiana na Watumishi ili kuweka mikakati imara ya kuendelea kupunguza kiwango cha upotevu wa maji.

Ametoa agizo hilo wakati akizindua Bodi ya Tisa ya Wakurugenzi wa DUWASA kwa niaba ya Waziri wa Maji. Tukio hilo lilihusisha kuiaga Bodi ya Nane iliyomaliza muda wake.

Amesema Bodi ya Nane kwa kushirikiana na Mamlaka wamefanya mambo mengi mazuri ikiwemo kupunguza upotevu wa maji hadi kufikia asilimia 28. Jukumu la bodi mpya ni kuhakikisha upotevu huo unafika chini ya asilimia 20.

Niwapongeze sana kwa kuweka jitihada kubwa za kupunguza kiasi cha maji yanayopotea, nimejulishwa kwamba wastani wa maji yanayopotea ni asilimia 28. Naiagiza bodi mpya kwa kushirikiana na Watumishi muweke mikakati ya kuendelea kupunguza kiasi hiki hadi kufikia chini ya asilimia 20” Mhandisi Mahundi amesema.

Tukio hilo limefanyika katika viwanja vya DUWASA Jijini Dodoma ambapo Mhe. Mahundi amesema Bodi iliyomaliza muda wake imefanya kazi nzuri ambayo imewezesha Mamlaka kuendelea kutoa huduma ya majisafi na kuwezesha ongezeko la watu baada ya serikali kuhamia Dodoma kuendelea kupata majisafi na salama.

Aidha, miradi mbalimbali imetekelezwa jijini Dodoma ukiwemo ujenzi wa tenki kubwa la Buigiri ambalo lina ujazo wa lita milioni 2.5. Amesema jukumu la Bodi ya Tisa ni kuhakikisha mafanikio haya yanasimamiwa na kuendelezwa, na thamani ya fedha iendelee kuonekana katika miradi inayoendelea kutekelezwa.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi za Mamlaka, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph amesema mamlaka imejipanga kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira ambapo tayari imefanya usanifu na inaendelea kubuni miradi ya muda mfupi, muda wa kati na mrefu itakayo boresha hali ya huduma katika maeneo mbalimbali yanayoyahudumiwa na Mamlaka hiyo.

Amesema kwa sasa kiwango cha maji yanayohitajika jijini Dodoma ni lita milioni 133 kwa siku na uwezo wa uzalishaji maji ni lita milioni 68.7 kwa siku. Uzalishaji huu ni takribani asilimia 50 ya mahitaji yote kwa siku hali ambayo imekuwa ikisababisha mgao wa maji.