Habari

Imewekwa: Mar, 20 2024

​Makamu wa Rais azindua mradi wa maji Hai, asisitiza utunzaji vyanzo vya maji

News Images

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amezindua mradi wa maji wa Kikafu-Bomangombe wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro wenye thamani ya ashilingi Bilioni 2.8. Mradi huo unatarajia kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji katika mji wa Hai ambao unajumuisha kata tatu za Bomang’ombe, Muungano na Bondeni kufikia asilimia 100.

Akizindua mradi huo Mhe. Mpango amewaagiza watendaji wa serikali kuhakikisha wanazuia vitendo vya uchomaji misitu ambavyo vimekuwa vikifanyika kandokando ya mlima Kilimanjaro na kuathili vyanzo vya maji. Amesema serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha huduma ya maji inamfikia kila mtanzania hivyo kila mtanzania anapaswa kutunza vyanzo vya maji ili viwe endelevu na kuzuia mabadiliko ya tabianchi.

Amewataka viongozi wa serikali kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa kusimamia na kuzuia shughuli za kibinadamu zinazoathili uendelevu wa vyanzo vya maji. kuhakikisha miti rafiki rafiki wa maji inapandwa katika maeneo yote yenye vyanzo vya maji.

Aidha Mhe. Mpango ameipongeza Wizara ya Maji kwa kutekeleza mradi na kubakisha fedha ambayo ameielekeza itumike kusambaza maji kwa wananchi wa eneo la Matowo.

Awali akiwazungumzia mradi huo Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema gharama za mradi huo kwa mjibu wa mkataba ilikuwa utekelezwe kwa gharama ya shilingi 3,392,463,389.08, kutokana na usimamizi mzuri mradi huo umekamilika kwa gharama ya shilingi 2,814,854,757.

Mhe. Jumaa Aweso amemhakikishia Mhe. Makamu wa Rais kwamba Wizara ya Maji itaendelea na jitihada za kuhakikisha inasimamia maagizo ili kuhakikisha kila kona ya nchi inafikiwa na huduma ya maji.

Amesema yako mafanikio ambayo wizara imeyapata ndani ya nje ya nchi ikiwemo kuwa ya kwanza katika utekelezaji wa miradi ya maji Duniani kupitia mradi wa Lipa kwa Matokeo (PforR) kwa miaka miwili mfululizo na kwamba mafanikio hayo watayaendeleza.

Amewaagiza watendaji wote nchini kuhakikisha wanasimamia ili wateja wapya wanaoomba kuunganishwa huduma ya maji waipate huduma hiyo ndani ya siku saba. Pia wahakikishe Ankara za maji zinakuwa halisia.

Makamu wa Rais Mhe. Mpango amezindua mradi wa maji Kikafu-Bomang’ombe ikiwa ni moja ya shughuli zinazofanyika katika kipindi cha wiki ya maji iliyoanza tarehe 16 mwezi huu. Kilele chake kinatarajia kuwa tarehe 22 mwezi huu ambayo pia ni Siku ya Maji Duniani.