Habari
Huduma ya maji inavyochochea Tanzania ya Viwanda Kibaha.
Mkoa wa Pwani unapakana na bahari ya Hindi. Majirani zake ni pamoja na mkoa wa Dar es Salaam ambao pia ni jiji maarufu la kibiashara hapa nchini Tanzania na ukanda wa kusini mwa Afrika. Kwa miaka ya hivi karibuni mkoa wa Pwani umekuwa na sifa ya ziada ya maendeleo ya viwanda. Zipo sababu nyingi zilizochochea haya, ikiwamo uwepo wa viwanda katika mji huo ikihusisha reli ya kisasa maarufu kama reli ya SGR ambayo inapita eneo hilo huku kukiwepo eneo la kimakakati la Bandari kavu ya Kwala pamoja na huduma ya majisafi na salama ambayo inatolewa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) mkoa wa Pwani pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Dar es Salaam (DAWASA).
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Wilayani Kibaha mkoani Pwani ni Mhandisi Debora Kanyika ambaye anasema Serikali ya awamu ya sita imeonesha nia ya dhati kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa kitovu cha maendeleo ya Viwanda na huduma nyingi kupitia uwekezaji mkubwa aliowekeza Mheshimiwa Rais kupitia huduma ya majisafi na salama.
Anasema huduma ya majisafi wilayani hapo sasa imewafikia wananchi kwa asilimia 78 huku jumla ya miradi mitano (5) ikiendelea kutekelezwa. Miradi hiyo itarajiwa kukamilika na kuongeza asilimia saba (7) ya huduma na kuifanya wilaya hiyo kufikia asilimia 85 ya huduma ya maji ambayo ni moja ya malengo yaliyoainishwa ndani ya ilani ya Chama cha Mapinduzi inayotekelezwa kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka 2025. Licha ya hatua hiyo, Mipango ya serikali inalenga kuhakikisha huduma ya maji inafikia asilimia mia moja na hivyo kuondoa kabisa changamoto ya huduma ya maji kwa wakazi wa Kibaha.
Anasema huu ni uthubutu mkubwa unaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amejipambanua kama mpambanaji ambaye anatambua adha kubwa wanayoipata akina mama wa Tanzania katika kutafuta huduma ya majisafi na salama.
Mhandisi Debora anamshukuru Rais kwa kujali wananchi wa eneo la Kibaha kwa kutekeleza miradi hiyo ambayo sasa inawezesha huduma ya maji kuyafikia maeneo yote muhimu ya kijamii pamoja na viwanda. Aidha anamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kusisitiza huduma hiyo isiishie kwenye maeneo ya biashara tu bali makazi ya watuna Taasisi za Kijamii ambapo sasa Mradi wa Kwala pekee umeweza kuzifikia Taasisi 9 katika eneo hilo.
“Mheshiwa Rais kwa kutambua umuhimu wa maji katika maeneo haya muhimu ameelekeza RUWASA kuhakikisha tunafikisha huduma ya maji katika maeneo hayo na kuyafanya yawe maeneo yenye kujitosheleza kwa upande wa maji. Hilo tumelitekeleza na tunaendelea kupambana kuhakikisha huduma ya maji inakuwa endelevu ili tusikwamishe jitihada za Rais katika nia yake ya dhati ya kuwatumikia watanzania.” Anasema Mhandisi Debora
Anasema zaidi ya shilingi Bilioni tano (5) zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji ikiwemo miradi sita yaMpiji, Minazi Mikinda, Kimara Misale,Ruvu station, Kwala na Mwembengozi,Kwala – bandari kavu na eneo la Uwekezaji (Dry Port na Sino Tan) pamoja na uchimbaji wa visima vitatu katika maeneo ya masaki, Kigoda na Miyombo.
Miradi hiyo imekuwa mkombozi na kuifanya Kibaha kuwa eneo lenye matumaini makubwa ya kukua kwa sekta mbalimbali zinazotegemea huduma ya maji. Mtandao wa mabomba katika wilaya sasa ni kilometa 193,995 ambazo zimewezesha kusambaa katika eneo kubwa la wilaya ya Kibaha ambayo inaundwa na tarafa mbili za Mlandizi na Ruvu zenye wakazi wapatao 123,367, hii ni kwa mjibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Mhandisi Debora anasema ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa endelevu, wilaya imeajiri wataalamu wenye weledi katika usimamizi wa miradi. Anasema Jumuia za watumia maji ni eneo muhimu ambalo wamelipa uzito kwa sababu ndio wanaohudumia walengwa kwa hiyo wameajili wataalamu wenye weledi na wenye elimu za kutosha kusimamia miradi.
Rose Mshana ambaye ni Mhasibu wa Chombo cha Watumia Maji Minazi Mikinda, anasema elimu yake ni Shahada ya kwanza ya Chuo Kikuu ambako amehitimu masomo ya Uhasibu. Anaishukuru Serikali kwa kuamua kuajili wataalamu kwani imeongeza tija katika usimamizi na kuongeza uzalishaji na uendelevu wa miradi. Pia imesaidia kupunguza tatizo la ajira kwa watanzania.
“Naishukuru serikali kwa kuwekeza katika sekta hii ya maji kwani imetusaidia sisi ambao tungeendelea kuwa mtaani bila ajira. Jumuia yetu ya watumia maji Minazi Mikinda inasonga mbele. Mapato ya mwezi yameonngezeka. Wataalamu wa serikali wanatukagua na kuridhika na usimamizi wetu wa miradi” anasema Rose.
Pia anatoa ushauri kwa serikali kuhakikisha inaendelea kuajiri wataalamu katika sekta zote za maendeleo ili kuondoa changamoto ya usimamizi na uendelevu wa miradi.
Kwa upande wake Manssoor Ally Kisabengo,Diwani wa kata ya Kwala ulipo Mradi wa maji Kwala ambao unahudumia Kongani ya Viwanda pamoja na bandari kavu ya Kwala anasema kala ya mradi wa maji wa Kwala hali ya huduma katika eneo lake ilikuwa ya shida sana.
“Mradi huu umekuwa mkombozi. Changamoto ilikuwa kubwa, tulikuwa tukiishi kwa kununua kwenye maboza na kuombaomba. Mradi uliokuwepo ulikuwa umechakaa sana, umechoka. Sasa shida ya maji kwala tumesahau. Tunamshukuru Rais na serikali kwa ujumla” Anasema Diwani Kisabengo na kuendelea kwamba sasa jamii ya Kwala imekuwa na ratiba nzuri ya maendeleo tofauti na zamani ambapo ratiba ya kutafuta maji ilikuwa ikiharibu mipango ya maendeleo. Aidha jitihada kubwa iliyopo sasa ni kuhakikisha wanaunganisha maji majumbani mwao. Vijana sasa badala ya kuhangaika kutafuta kazi ya kusomba maji, sasa jitihada ni kazi ni viwandani.
Naye Fatuma Matambi, mkazi wa Kwala anapongeza serikali na kusema sasa jamii imependeza na kung’aa kwa sababu ya ujio wa maji. Anasema kabla ya ujio wa mradi wa maji Kwala, ilikuwa ikiwalazimu kununua maji shilingi mia tano kisha kuingia gharama za bodaboda kwa shilingi elfu moja kwa kila ndoo ya maji. sasa yote hayo yamekuwa historia kutokana na uthubutu wa dhati wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia suluhu Hassan ambaye ameamua kwa dhati kumtua mtanzania kutoka kwenye adha ya maji.
Hatua hizi zote za Serikali kuwafikia wananchi na wawekezaji zinabeba ule msemo wa Waziri wa Maji Jumaa Aweso (Mb) ukiwa na mgonjwa, mihemo yake unaipata sawasawa, kwa maana Serikali imewashirikisha wananchi na kuelewa kiu yao katika huduma muhimu ya maji.