Habari

Imewekwa: Aug, 23 2024

​Hati Fungani ya Tanga kutinga soko la Hisa la Luxembourg

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewasilisha taarifa kuhusu hati fungani ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.

Mhe. Aweso amesema Wizara ya Maji imekuwa na ubunifu wa aina mbalimbali lengo likiwa kuhakikisha azma ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi inafikiwa kwa haraka zaidi na kwa viwango vinavyostahili.

Amesema hati fungani hiyo tayari imesajiliwa katika soko la hisa la Dar es salaam, na kuwa Taasisi ya kwanza ya umma inayotoa huduma katika jamii kuingia katika soko hilo. Aidha hati fungani hiyo imevutia mataifa mbalimbali ambapo mwezi Oktoba 2024 inatarajiwa kuingia rasmi katika soko la hisa la nchi ya Luxembourg baada ya mawasiliano kati ya Wizara ya Maji na soko la hisa la Luxembourg barani Ulaya kufikia muafaka.

Amesema Luxembourg wamefurahishwa na mwendo usiotia shaka wa Wizara ya Maji katika kusimamia na kuendeleza sekta ya maji. Pia Sera nzuri za nje za Tanzania ambazo zinasimamiwa vizuri na serikali ya awamu ya sita.

Wajumbe wa kamati wamepongeza hatua hiyo na kuzitaka Mamlaka nyingine za maji kuiga mfano huo. Wamesema fedha kutoka serikali kuu haziwezi kutosheleza mahitajhi yote ya taasisi na hivyo ubunifu wenye kulenga kutafuta fedha kwa njia zingine tofauti utasaidia Kusukuma maendeleo ya sekta ya maji na kuyafikia malengo kwa wakati.

Tanga UWASA inakuwa taasisi ya kwanza inayotoa huduma kwa umma kuingia katika soko la la hisa kwa nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano na darasa kwa nchi nyingine.