Habari

Imewekwa: Jan, 17 2025

Aweso akutana na Katibu Mtendaji Baraza la Mawaziri wa maji Afrika

News Images

Waziri wa maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amefanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika (African Ministers’ Council on Water-AMCOW).

Mazungumzo yamefanyika katika Ofisi za Wizara ya Maji, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Menejimenti ya Wizara.

Mazungumzo hayo yamehusu Maandalizi ya Dira ya Maji ya Afrika (Africa Water Vision 2050); pamoja na Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika Kanda ya Afrika Mashariki ambao unatarajia kufanyika Machi 4-7, 2025.

Mhe. Aweso amemshukuru Katibu Mtendaji na kuahidi ushirikiano wa kutosha kutoka Tanzania katika utekelezaji wa maagizo yote ambayo yamekuwa yakitolewa na baraza hilo la mawaziri.

Amesema tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani ameonesha nia ya dhati ya kuhakikisha Sekta ya Maji inapiga hatua.

Aidha, ametumia fursa hiyo kufikisha ujumbe kwa AMCOW akiomba AMCOW kushirikiana na Tanzania katika malengo yake ambayo ni pamoja na kupata mtandao wa maji wa Taifa.

“Napenda kukufahamisha kuwa Tanzania ipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi wa mtandao wa maji wa Taifa (National Water Grid). Hii itafanya Tanzania kuyafikia maeneo mengi zaidi katika huduma ya maji na hivyo kusukuma mbele maendeleo ya Taifa, Niwaombe AMCOW mtuunge mkono katika eneo hili.” Aweso amesema.

Pia, AMCOW kuendelea kuungana na Tanzania katika utekelezaji wa program mbalimbali zinazohusisha usimamizi na uendelezaji wa Rasilimali za maji, ujenzi wa miradi ya maji na usambazaji maji.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na ushirikiano mzuri. Amesema Tanzania ambayo ni mwanachama wa AMCOW itashika nafasi ya Makamu wa Rais wa AMCOW Kanda ya Afrika Mashariki inayojumuisha nchi za Tanzania, Burundi, Djibuti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini na Uganda mwezi Februari 2025 na kwamba hakuna mashaka na utayari wa serikali ya Tanzania.

Ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika maeneo mbalimbali kwani anajua maji ni uhai na ni nyenzo muhimu katika kusukuma maendeleo ya sekta mbalimbali katika jamii.