Habari
Ahadi ya Rais Samia Yatekelezwa Jijini Arusha

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameshuhudia utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya maji yanayotoka Valesca Mbuguni kufika Jijini Arusha kwa lengo la kuboresha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi.
Rais Samia alitoa ahadi hiyo ya maji kutoka chanzo vya Valesca Mbuguni kufika Jijini Arusha ifikapo mwezi Disemba, 2021 wakati akizungumza na wakazi wa Chekereni mwezi Oktoba 17, 2021 wakati alipotembelea mradi wa maji wa Jiji la Arusha katika kituo cha kusukumia maji kilichopo eneo la Chekereni ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Arusha wenye thamani ya Sh. Bilioni 520.
Mhandisi Sanga amesema kazi ya kufikisha maji hayo na kuingia kwenye mfumo imetekelezwa na kilichobaki ni kuongeza mtandao na kufikisha maji hayo kwa wananchi wengi iwezekanavyo, ambapo awali maji kutoka chanzo cha Seed Farm yalishafika na kutoka chanzo cha maji Majimoto yanatarajiwa kufika hivi karibuni.
Katibu Mkuu Sanga ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (AUWSA) kuhakikisha maji yote yanayozalishwa hayapotei kwa kuthibiti mivujo ili wananchi wapate huduma inayotosheleza mahitaji wakati wote na kukamilisha utekelezaji wa mradi wote ifikapo mwezi Juni, 2022.
Aidha, amesisitiza kuwa maji ya mradi huo yatahudumia mpaka vijiji na kusema kuwa mpaka sasa usanifu wa miradi kwenye vijiji 5 umeshafanyika na kumtaka Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Arusha kuongeza idadi ya vijiji zaidi ili viweze kunufaika.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA), Mhandisi Justine Rujomba amesema maji hayo yataongeza uzalishaji wa lita milioni 26 kwa siku na sasa wanaendelea majaribio na kusafisha mabomba.