Habari

Imewekwa: Mar, 09 2019

Wizara Haitolipa Fedha Zozote Kwa Wakandarasi Bila Kujiridhisha na Kazi Zao- Naibu Waziri wa Maji

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso ametamka kuwa wizara haitalipa fedha zozote bila kujiridhisha na kazi inayofanywa na mkandarasi, bali italipa madai ya wakandarasi kulingana na kazi wanazozifanya.

Aweso amesema hayo wakati alipokuwa wilayani Bahi kukagua Mradi wa Maji wa Mkakatika mkoani Dodoma kutokana na hoja mkandarasi ya kulipwa malipo ya awali wakati akifuatilia utekelezaji wa miradi wilayani humo.

Akizungumza mbele ya wananchi amesema utaratibu wa wizara ni kufanya malipo mara baada ya mkandarasi kuwasilisha hati zake za madai kuendana na mpango wa kazi.

‘‘Utaratibu wetu kwa kawaida baada ya kupokea hati ya madai kwanza tunajiridhisha na kazi iliyofanyika, kama inalingana na madai yaliyowasilishwa na mkandarasi, baada ya hapo ndipo tunaidhinisha malipo hayo mara moja ukizingatia fedha zipo’’, Naibu Waziri Aweso amesema.

‘‘Rai yangu kwa wakandarasi wote wenye kazi za miradi ya maji nchini, wizara haitakuwa tayari kutoa fedha za awali kabla ya kazi yoyote kufanyika. Hakikisheni mnafanya kazi kwanza usiku na mchana na kuleta madai yenu wizarani tutawalipa’’, Naibu Waziri Aweso amesema.

Akifafanua kuwa kulikuwa na utamaduni hapo awali wa kutoa fedha za awali ambazo ni asilimia 15 ya jumla za gharama za mradi kwa wakandarasi na matokeo yake wengi wao wakawa wanazitumia kwenye kazi zao nyingine, hali iliyosababisha miradi ya maji kukwama pamoja na kulipwa fedha hizo.

Akiahidi kuwa atafuatilia hati za madai za wilaya hiyo za miradi ya Kigwe-milioni 100, Magaga-milioni 131 na visima virefu-milioni 206 zilizowasilishwa wizarani na kama ni sahihi zitalipwa zote ili miradi hiyo iweze kukamilika na kusaidia wananchi wa Bahi.

Aidha, Aweso ametoa siku nne tenki la maji la Mradi wa Mkakatika liwe limeshanunuliwa na kufungwa na kuagiza ufanyike utaratibu wa kisheria Kamati ya Maji ya Mkakatika ivunjwe kwa kuwa imeshindwa kufanya kazi ya kuusimamia mradi huku wananchi wakiendelea kupata tabu, wakati akaunti ya kamati hiyo ikiwa na zaidi ya shilingi milioni 6.

Vilevile, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nipo African Engineering, Mhandisi Marcus Gondwe kwa kazi nzuri inayofanywa na mkandarasi huyo na kusema wizara itampa ushirikiano unaostahili ikiwemo kumlipa fedha zake kwa wakati ili aweze kukamilisha mradi.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Mukunda amemshukuru Naibu Waziri Aweso kwa kukubali ombi lake la malipo ya fedha za mkandarasi kwa maslahi mapana ya Bahi na kumuagiza Kaimu Mhandisi wa Maji Wilaya ya Bahi, Bw. Hafidh Juma kusimamia kazi hiyo.

Mradi wa Maji wa Mkakatika ni miongoni mwa miradi 6 ya visima virefu inayotekelezwa katika Wilaya ya Bahi katika Mwaka wa Fedha 2018/19, mkataba wake ulisainiwa Agosti 23, 2018 na unatarajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi milioni 637.