Habari

Imewekwa: Mar, 01 2019

Wiki ya Maji kuadhimishwa Kitaifa Mkoani Dodoma

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) leo akiwa katika ofisi yake ndogo ya Dar es Salaam amezungumza na vyombo vya habari kuujulisha umma kuhusu maadhimisho ya siku ya maji ambayo yatakayoanza tarehe 16 Machi na kuhitimishwa tarehe 22 Machi, 2019.

Kitaifa maadhimisho haya yatafanyika katika mkoani Dodoma.

Waziri Mbarawa amesema shughuli mbalimbali zimepangwa kufanyika, ikiwemo mikutano, warsha, semina, maonesho, pamoja na ukaguzi na uzinduzi wa miradi ya maji.

Hata hivyo, amesema pamoja na shughuli mbalimbali zitakazofanyika nchi nzima, ikiwemo ukaguzi na uzinduzi wa miradi ya maji, mikutano mitatu imepangwa kufanyika kama ifuatavyo:

a) Tarehe 18-19 Machi 2019: Mkutano wa kitaifa wa mwaka wa maji utakaoshirikisha wadau na wataalamu wa maji (Annual Water Scientific Conference) utakaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya St. Gaspar Jijini Dodoma. Katika mkutano huu wadau wa sekta ya maji watawasilisha na kujadlili mada mbalimbali zinazohusu matokeo ya tafiti, utunduizi na ugunduzi mbalimbali katika sekta ya maji;

b) Tarehe 20-21 Machi 2019: Siku maalum ya EWURA (EWURA Day) nayo itafanyika katika hoteli ya St. Gaspar jijini Dodoma. EWURA itazindua na kuwasilisha Ripoti ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini kwa mwaka 2017/18

c) Tarehe 22 Machi, 2019: Katika kuhitimisha maadhimisho ya wiki ya maji kutakuwa na Mkutano wa Mapitio ya Sekta ya Maji (Joint Water Sector Review). Mkutano huu ni maalumu kwa wadau kutathmini utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) nchini.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Hakuna Atakayeachwa: Kuongeza Kasi ya Upatikanaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa Wote katika dunia inayobadilika kitabia nchi” (Leaving No One Behind: Accelerating universal access to water supply and sanitation services in a changing climate).

Pia mbali na maadhimisho katika ngazi ya kitaifa, maadhimisho ya wiki ya maji yatahusisha shughuli mbalimbali katika ngazi za mikoa na halmashauri. Hivyo, ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ofisi za Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini na Ofisi za Bodi za Maji za Mabonde zinahimizwa kushiriki kikamilifu katika kuadhimisha wiki ya maji kwa kufanya shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta ya maji, kama kushirikisha wananchi kupanda miti katika maeneo ya vyanzo vya maji; kufanya uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi ya maji iliyokamilika kwa kuwashirikisha viongozi waliopo katika maeneo yao; kutoa elimu ya umma kuhusu mikakati ya ulinzi, utunzaji na uendelezwaji wa raslimali za maji, vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla na kujadili mafanikio na changamoto zilizopo katika utekelezaji wa miradi ya maji na utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi; pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao.