Habari

Imewekwa: Jan, 24 2019

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akagua Miradi ya Maji katika Halmashauri ya Kongwa na Chamwino

News Images

Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa amefanya ziara ya kikazi Wilaya ya Kongwa na Chamwino ili kukagua miradi ya maji inayoendelea kwenye maeneo mbalimbali katika Wilaya hizo.

Profesa Mbarawa ameridhishwa na kazi za ujenzi wa miradi katika wilaya hizo na ameahidi kulipa hati za madai wanazodai wakandarasi zilizofikishwa Wizarani kwake.

Akiwa katika ziara hiyo Mbunge wa Kongwa na Spika wa Bunge la Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai amemuomba Waziri Mbarawa kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kibaigwa kwa kushindwa kuisimamia Mamlaka hiyo.

Aidha, Waziri Mbarawa aliivunja Bodi ya Mamlaka ya Maji Kibaigwa baada ya kujiridhisha kushindwa kufanya kazi kwa weledi. Mamlaka hiyo pia ilikopa fedha kwa ajili ya kununua pampu iliyoharibika kutoka Mamlaka ya mji mdogo wa Kibaigwa jambo ambalo pia halijampendeza Spika Ndugai na Waziri Mbarawa.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Mbarawa alitoa ahadi ya kulipa deni la shilingi milioni 25 kwa ajili ya pampu zilizoharibika na kutoa onyo kali kwa Meneja wa Mamlaka na kumtaka abadilike kwa kuwa hata toa pesa kwa ajili ya Mamlaka hiyo kwa vitu vidogo vidogo tena.

Pia Waziri Mbarawa amemuagiza meneja huyo kupandisha makusanyo kutoka wastani wa shilingi milioni 35 hadi milioni 52 kwa mwezi ili iweze kujiendesha.

Akiwa Wilayani Chamwino Profesa Mbarawa alisomewa taarifa ya maji na baadae aliwaahidi kuwa atahakikisha wakazi wa Chamwino wanapata maji safi na salama kwa haraka na atafatilia kwa karibu miradi yote inayoendelea katika Halmashauri hiyo.