Habari

Imewekwa: Jan, 31 2019

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa azindua Bodi ya Maji ya Taifa

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa (Mb) leo amezindua Bodi ya Maji ya Taifa jijini Dodoma.

Profesa Mbarawa akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Maji ameitaka Bodi mpya ya Maji ya Taifa kubadilika na kufanya kazi kwa ufanisi, weledi na uadilifu ili kusimamia rasilimali za maji nchi ambazo haziongezeki.

Profesa Mbarawa, pamoja na kazi nyingine, ameiagiza bodi hiyo kuangalia sheria na kanuni mbalimbali kuhusu matumizi ya rasilimali maji kama zina tija na kuendana na mabadiliko yanayoendelea Duniani, pia kuwa na manufaa kwa wananchi ili wapate maendeleo kupitia rasilimali maji.

Kuhusu makusanyo, Waziri Mbarawa amesema, Mabonde yote tisa (9) nchini yanapaswa kukusanya maduhuli kupitia vyanzo mbali mbali kwa mujibu wa sheria ili ziwe na uwezo mkubwa wa kujiendesha badala ya kuitegemea serikali kuu kifedha kwa kila jambo.

Wizara ya Maji katika kuiwezesha Bodi ya Taifa ya Maji ili kufanya kazi yake kwa ufanisi, imeanza maandalizi ya kuunda Kituo Mahiri cha Rasilimali za Maji (Water Resources Centre of Excellency) ambacho kitakuwa na wataalam kutoka sekta mbalimbali ili kufanya utafiti (studies) na uchambuzi wa takwimu za rasilimali za maji na mipango ya usimamizi wa rasilimali hizo.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo amesema kuwa Sheria za Maji za Tanzania zimeainisha mfumo madhubuti wa usimamizi rasilimali za maji unaoshirikisha wadau kuanzia ngazi ya chini ya watumiaji maji (Water users associations), ngazi za mabonde na ngazi ya Taifa ambayo ndiyo chombo cha juu cha kumshauri Waziri wa Maji.

Bodi ya 3 ya Maji ya Taifa itaongozwa na Profesa Hudson Hamisi Ngotagu na wajumbe wafuatao ambao walihudhuria uzinduzi huo:-

  • Dr. George Lugomela – Katibu
  • Mhandisi Juma Mkobya – Mjumbe
  • Bw. Deogratius P. Nyangu – Mjumbe
  • Mhandisi Wilhelmina Malima – Mjumbe
  • Mhandisi Anna Mwangamilo – Mjumbe
  • Bw. Emmanuel Bulayi -Mjumbe
  • Dkt. Andrew Komba – Mjumbe
  • Bw. Hussein S. Ally – Mjumbe

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano

30 Januari, 2019