Habari

Imewekwa: Dec, 06 2018

Waziri wa Maji Aridhishwa na Maendeleo ya Mradi wa Maji Kiwalani

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa ameridhishwa na maendeleo ya Mradi wa Maji Kiwalani baada ya kukuta maeneo mengi yakinufaika na mradi huo.

Ametoa kauli hiyo mara baada ya kufika kwenye mradi huo ili kujua manufaa ya mradi huo kwa wananchi mara baada ya uzinduzi wa mradi huo miezi michache iliyopita.

Profesa Mbarawa amesema kuna tabia miradi imekuwa ikitoa maji vizuri baada ya kuzinduliwa, baada ya hapo kunakuwa hakuna kinachoendelea na kukosa tija.

Akisisitiza ile kuwe na miradi yenye tija na kunufaisha wananchi, ni lazima kuwe na utaratibu wa ufuatiliaji wa mara kwa mara na kujua maendeleo yake.

"Nia yangu ni kupata mrejesho kutoka kwa wananchi baada ya kupata mradi huu, maeneo mengi yanapata maji na wananchi wamenithibitishia hilo, pamoja na watu wachache kuhujumu mradi huu", amesema Profesa Mbarawa.

Amesema kuna baadhi ya watu wenye maslahi binafsi wamekuwa na tabia ya kuchafua maji yanayosambazwa kwa wananchi na kusababisha wakati mwingine maji kuwa machafu.

Amevitaka vyombo vya usalama vifanye uchunguzi na kuwachukulia hatua pindi watakapowakamata wahusika, kwa kuwa Serikali haitalifumbia macho jambo hilo.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kaluwa amesema mradi huo umekuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Kiwalani, pamoja na changamoto ndogo ndogo na kuiomba Serikali izidi kuimarisha huduma ya maji Kiwalani na Segerea kwa ujumla.