Habari

Imewekwa: Dec, 07 2018

Waziri Mbarawa Ataka Kero ya Maji Mtoni Itatuliwe

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa ametaka kero ya maji kwa wakazi wa Mtoni itatuliwe haraka iwezekanavyo mara baada kujionea hali huduma ya maji kwa wananchi.

Amezungumza hayo katika muendelezo wa ziara yake ya kusiskiliza kero za wananchi jijini Dar es Salaam, na kuitaka DAWASA itafute suluhisho la kufikisha huduma ya maji kwa wananchi, ukizingatia uwepo wa chanzo cha maji na mtambo wa kusafishia maji katika eneo la Mtoni.

Profesa Mbarawa amesema haoni sababu ya wananchi hao kukosa maji kwa kuwa kuna chanzo cha maji cha uhakika, kinachohitajika ni kuweka mkakati mzuri wa ujenzi wa miundombinu itakayofikisha maji kwa wananchi kwa kuwa chanzo kipo.

Akiwa kwenye Mtaa wa Mashine ya Maji, Profesa Mbarawa amekutana na kero ya maji kutoka kwa wananchi ambao wamesema maji wanayotumia yanayotoka kwenye kisima usalama wake ni mdogo, kumuomba Waziri wa Maji awatatulie changamoto hiyo.

Aidha, wamemuomba Waziri wa Maji aipatie ufumbuzi changamoto ya kisima kilichochimbwa na Halmashauri ya Temeke kilichokuwa kikitumika awali kwa ajili ya kutoa huduma ya maji kwa wananchi kuhodhiwa na mtu binafsi wakati wao wakiwa na uhitaji mkubwa wa maji.

Akijibu hoja za wananchi hao Profesa Mbarawa amesema atatuma timu ya wataalamu wa DAWASA ifike eneo hilo Jumatatu ijayo, ili waweze kufuatilia jambo hilo kabla ya kuchukua hatua zinazostahili. Pia, waangalie namna jinsi watakavyoweza kufanikisha zoezi la kufikisha huduma ya maji kwa wakazi hao.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amemaliza ziara yake ya siku tano katika Jiji la Dar es Salaam; ambapo ametembelea maeneo yenye changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji ya Kimara, Bonyokwa, Salasala na Mtoni kusikiliza kero za wananchi ambazo amekuwa akizisikia kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi. Pamoja na Kiwalani ambapo alikwenda kupata mrejesho kutoka wa wananchi kuhusu maendeleo ya Mradi wa Maji Kiwalani uliozinduliwa hivi karibuni.