Habari

Imewekwa: Jun, 15 2019

Waziri Mbarawa Amuweka Ndani Mkandarasi

News Images

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amekasirishwa na utendaji kazi wa Mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Mkwiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba na kuamuru Mkandarasi wa Kampuni ya Mshamindi Construction Limited and Edge Pont Company Ltd kukamatwa na kuwekwa ndani mara moja.

Waliowekwa ndani ni Bwana Fadhil Salum, Charles Kilosa na Raymond Mwanache wote wametoka katika kampuni ya Mshamindi Construction Limited and Edge Pont Company Ltd.

“Hakikisheni mnawaweka ndani na tutawatoa nje pale watakapoleta barua ya kukubali kuonesha kazi ya kulaza mabomba wataimalizi lini na kwa muda mfupi” alisema Waziri Mbarawa.

Waziri amechukua hata hiyo baada ya Mkandarasi huyo kushindwa kukamilisha kazi ya kutekeleza mradi wa Mkwiti wa Wilaya ya Tandahimba wenye thamani ya shilingi bilioni 8.5 ambao unatakiwa ukamilike Desemba, 2019 baada ya kuongezewa muda mwingine wa miezi 3.

Mradi huu ukikamilika utahudumia vijiji 14 ambavyo ni Mangombya, Nannala, Nanjanga, Chidede, Ngunja, Mkwiti juu, Mkwiti chini, Mabeti, Litehu, MMeda, Likolombe juu, Namindondi juu, Namindondi chini na Mkola juu na wananchi wapatao 21,384 watapata maji safi na salama na upatikanaji wa maji Wilaya itaongezeka kwa asilimia 9.39.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Bwana Sebastian Waryuba amemshukuru sana Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kwa uamuzi wake wa kizalendo wa kuwachukulia hatua Wakandarasi hao kwani wananchi wa Tandahimba na Newala wanahitaji huduma ya maji na siyo ubabaishaji unaofanywa na Kampuni hiyo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

15.6.2019