Habari

Imewekwa: May, 03 2018

NAIBU WAZIRI AWESO AKAMATA WEZI WA MAJI MOROGORO

News Images

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amekamata Kiwanda cha Nguo cha 21st Century kilichopo mkoani Morogoro kwa wizi wa maji, alipofika kiwandani hapo kwa kushtukiza mara baada ya kupata taarifa kuwa kinafanya wizi wa maji na kuihujumu Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA).

Naibu Waziri Aweso amefika na kujionea wizi unaofanywa na kiwanda hicho na kuikosesha MORUWASA mapato sahihi kwa kung’oa mita za maji zinazotoa taarifa za matumizi kila zinapofungwa.

‘‘Hii ni mara ya tatu sasa wakifungiwa mita wanazing’oa, huu ni wizi ambao ninausema kila siku. Kiwanda hiki kinapewa huduma ya maji kwa ajili ya shughuli zake za uzalishaji lakini kinakwepa kulipa gharama, jambo hili si sahihi na sitakubali mchezo huu uendelee’’, amesema Aweso.

Amesema kuwa wanavithamini sana viwanda vyote nchini, hususan katika kuiunga mkono dhana ya kuwa na uchumi wa viwanda lakini, viwanda hivyo vina wajibu wa kufuata taratibu na sheria za nchi ikiwemo kulipia gharama za huduma ya maji na si kuhujumu mapato ya Serikali.

‘‘Huu ni mwanzo tu, nimepata taarifa nyingi kuhusu viwanda vilivyounganishiwa maji maeneo mbalimbali nchini bila kulipa gharama zozote, tutaendelea kuwafichua na kuwakamata ili wafikishwe mbele ya sheria lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kuinua Sekta ya Maji ili wananchi wote wapate maji’’, amesema Aweso.

Naye Bertam Minde wa Kitengo cha Upotevu wa Maji Yasiyolipiwa cha MORUWASA, amesema Manispaa ya Morogoro ina changamoto kubwa ya wizi wa maji, pamoja na juhudi za kukomesha tatizo hilo na kuiomba wizara kuendelea kuwapa ushirikiano wa karibu ili kukabiliana na tatizo hilo.

Akizungumza Mkurugenzi wa MORUWASA, Mhandisi Nicholaus Angumbwike amesema wamekuwa wakikosa mapato mengi kutokana na kuhujumiwa na watu wasio waaminifu na kuipa mamlaka wakati mgumu kujiendesha, wamejipanga kuunda kikosi maalum kwa ajili ya kushughulika na hujuma zote.

Katika tukio hilo Meneja wa Fedha, Jayesh Vaidya na Meneja Uzalishaji, Clement Munisi wa kiwanda hicho walikamatwa na polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.