Habari

Imewekwa: Oct, 24 2018

Waziri Aweso Aelekeza Timu ya Wataalam wa Maji wa Wizara ya Maji Kukagua Miradi ya Maji Wilayani Mbulu

News Images

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameelekeza timu ya wataalam wa maji kutoka Wizara ya Maji kukagua miradi yote ya maji katika wilaya ya Mbulu mkoani Manyara na kuainisha changamoto za miradi hiyo na namna ya kuzimaliza ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama kama Serikali ilivyopanga.

Mhe. Aweso ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya kikazi katika Wilaya ya Mbulu ambapo amekagua mradi wa maji wa Arri, mradi wa maji Mongahay – Tumati, na mradi wa maji Dongobesh.

Mhe. Aweso (Mb) amesema miradi hiyo imechukua muda mrefu kukamilika wakati wananchi wanapata adha ya kutokua na uhakika wa majisafi na salama kwasababu mahitaji yameongezeka. Amesema baadhi ya miradi wamepewa wakandarasi wasio na uzoefu wa kutosha hivyo kushindwa kuikamilisha kama kwa mujibu wa mikataba waliyopewa.

Waziri Aweso (Mb) akiongea na wakazi wa Mbulu amesema hatavumilia kuona rasilimali za serikali zinatumika vibaya katika sekta ya maji, na kuainisha kuwa wakandarasi wanaoharibu miradi ya maji, watachukuliwa hatua za kisheria, pamoja na kufungiwa kushiriki kazi yoyote inayohusu sekta ya maji hapa nchini.

Pamoja na hilo, Mhe. Aweso (Mb) ameelekeza Jumuiya za Watumia Maji nchini zisajiliwe, na ziweke mikakati ya kutunza miradi ya maji ili idumu na kuwa endelevu. Aidha, viongozi wawashirikishe waanchi kulinda vyanzo vya maji na watoe elimu zaidi ili kuzuia kazi ya aina yoyote katika vyanzo vya maji ndani ya umbali wa mita 60. Aidha, Mhe. Aweso (Mb) ameagiza fedha za dharura kiasi cha shilingi milioni 60 zitumike kuchimba kisima cha maji kwa wakazi wa Haydom.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Maji.

24.10.2018