Habari

Imewekwa: Mar, 23 2019

Watendaji Mamlaka za Maji Watakiwa Kuongeza Uwajibikaji

News Images

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo amesema watendaji wa mamlaka za maji watakaoshindwa kulipa tozo mbalimbali kwa wakati watawajibishwa kwa uzembe katika kazi.

Profesa Mkumbo amesema hayo wakati akihitimisha Wiki ya maji kwa mwaka 2019 na Mkutano wa Mapitio ya Sekta ya Maji (Joint Water Sector Review) jijini Dodoma. Tozo zinatakiwa kulipwa katika bodi za mabonde mbalimbali ambako mamlaka zina vyanzo vya maji na tozo za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Hata hivyo, ameainisha kuwa endapo tozo hizo ni kubwa watendaji wa mamlaka za maji wanatakiwa kusema na kuwataka kulipa tozo kwa wakati kwani ni moja kati ya vigezo vya kupima utendaji kazi katika mikataba iliyosainiwa kati ya Watendaji wa Mamlaka za maji na Wizara ya Maji mapema mwezi Machi, 2019 jijini Dodoma.

Pamoja na hayo, Prof. Mkumbo amesema miongoni mwa mambo ambayo watendaji wa mamlaka za maji wanayotakiwa kuyapa uzito ni suala la upotevu wa maji (NRW). Amesema jambo hilo ni kero na linapoteza mapato, na pia huduma kwa wananchi inakua ya kusuasua katika baadhi ya maeneo kwa sababu maji yanapotea. Eneo jingine la msisitizo ni suala la usafi wa mazingira ambapo mipango mizuri inatakiwa kuwekwa na mamlaka zote kwa kuzingatia mipango ya biashara.

Prof. Mkumbo kupitia wiki ya maji amewapongeza Washirika wa maendeleo kwa ushirikiano mzuri na Serikali, pamoja na AZAKI ambazo zinapaza sauti kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu huduma ya maji kwa wananchi. Amesema yote wanayoshauri yanachukuliwa na kufanyiwa kazi na Serikali kwa sababu wananchi ndio wadau namba moja wa Serikali.

Kaulimbiu ya wiki ya maji 2019 ilikuwa ni “Hakuna Atakayeachwa: Kuongeza Kasi ya Upatikanaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa Wote katika Dunia inayobadilika kitabia nchi”

Mwaka 1993 Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira na Maendeleo lilipitisha Azimio rasmi la kuadhimisha Siku ya Maji Duniani kila mwaka ifikapo tarehe 22 Machi.

Wizara ya Maji imekua ikiratibu na kuadhimisha siku hii muhimu kuanzia mwaka 1988. Haya yamefanyika kwa kuwashirikisha wananchi na wadau wa maji. Lengo kuu likiwa kuungana na Mataifa mengine Duniani katika kutathmini utekelezaji, mafanikio, changamoto na kuainisha mikakati ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira na kusimamia utunzaji wa rasilimali za maji.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

23.03.2019