Habari

Imewekwa: Feb, 27 2019

Wananchi wa Mkoa wa Tanga Waagizwa Kutunza Vyanzo vya Maji

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) amewataka wananchi wa mkoa wa Tanga kutunza vyanzo vya maji ili viwe endelevu kwa matumizi ya sasa na kizazi kijacho. Pia amewataka watunze miundombinu ya maji na kulipia huduma ya maji kwa wakati.

Waziri Mbarawa aliyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi mkoani Tanga, ambapo alikagua miradi ya maji na kuongea na wananchi kuhusu huduma ya maji.

“Hakikisheni mnatunza vyanzo vya maji na kuvilinda, tusipofanya hivyo itakuwa tunafanya kazi bure hata hiyo miundombinu ambayo tunaijenga kwa gharama kubwa haitasaidia kwasababu maji hayatakuwepo bila kutunza vyanzo vyetu vya maji”, Waziri Profesa Mbarawa alisema.

“Hali ya upatikanaji wa maji katika Halmashauri ya Kilindi, Mkinga, Korongwe, Handeni hairidhishi hivyo basi serikali inafanya jitihada za makusudi ili wananchi wa maeneo haya waweze kupata majisafi na salama na yakutosha” Prof. Mbarawa alisema.

Akiwa wilayani Kilindi Waziri Mbarawa alijionea ujenzi wa tanki la maji ukiwa umekamilika lakini pampu imeungua hivyo wananchi kukosa huduma ya maji. Kufuatia hilo, mkandarasi aliyetekeleza mradi huo alipewa muda hadi Ijumaa ya tarehe 1 Machi, 2019 awe ameshafunga pampu nyingine, na kurejesha huduma ya maji kwa wananchi.

Waziri Mbarawa alisema katika maeneo mengi aliyopita ameona kuwa changamoto kubwa ya miradi ya maji inasababishwa na wataalam kwa sababu wanawapa fursa Wakandarasi kufanya chochote wanachotaka, hivyo amewataka wataalam kuwa waadilifu na kusimamia miradi kwa ukaribu zaidi.

Aliongeza kuwa Wizara ya Maji ipo katika mchakato wa kuanzisha Wakala ya Maji Vijijini na kusisitiza hatua hiyo italeta tija zaidi.

Wakati huohuo, Waziri Mbarawa akiwa katika mji wa Mombo aliahidi wizara yake kutoa kiasi cha shilingi milioni 500 kwa Mkandarasi aitwaye Saxon Building ili kumuwezesha kuendelea na ujenzi wa mradi wa maji wa Rwegela na Msambiazi iliyopo Korogwe mjini.

pamoja na hayo, Waziri Mbarawa katika ziara hiyo alipata fursa ya kuongea na wananchi kupitia radio ya kupokea maoni na hoja mbalimbali kuhusu huduma ya maji mkoani Tanga haswa katika Halmashauri za Mkinga na Handeni ambapo aliahidi kuzifanyia kazi kwasababu ameziona kwa kutembelea maeneo husika na lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata majisafi, salama na yenye kutosheleza karibu na makazi yao