Habari

Imewekwa: Mar, 08 2019

Wakala ya Maji Vijijini (RUWASA) Kutatua Changamoto za Maji Vijijini

News Images

RUWASA iliyotokana na Sheria mpya ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2019 iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge iko katika hatua za uundwaji inategemea kuanza hivi karibuni mara baada ya taratibu zote za muundo na kiutendaji kukamilika.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa ametamka hayo wakati akizungumza na Watendaji wa Sekta ya Maji nchini katika kikao kazi kilichohusu kujenga uelewa wa muundo wa RUWASA na utendaji wake katika kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho Profesa Mbarawa amesema kutokana na shida zilizobainishwa kutokana na sheria za zamani, ilibidi wizara ihuishe kwa kuwa sheria moja itakayomaliza changamoto zote; itayoangalia na kusimamia huduma ya majisafi na usafi wa mazingira nchini.

Dhumuni la sheria hii ni kuongeza uwajibikaji mkubwa kwa watendaji na kutatua changamoto za maji vijijini, utoaji wa huduma ya majisafi na salama na uchimbaji wa visima.

"Sheria hii imekuja na uanzishwaji wa RUWASA ambayo itasimamia utekelezaji wa maji vijijini na kutoa mwongozo wa usimamizi wa miradi ya maji vijijini ambayo imefikia asilimia 59.8 kwa sasa", amesisitiza Profesa Mbarawa.

"Tunaendelea na utekelezaji unaoigharimu Serikali mabilioni ya shilingi kwenye miradi ya Arusha Mjini, Same-Mwanga-Korogwe, Longido na Nzega-Igunga-Tabora na yote ikikamilika tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa sana kero ya maji kwa wananchi.

"Vilevile tunaendelea kuona maendeleo makubwa kwenye mamlaka za maji nchini kama DUWASA, MWAUWASA, Tanga UWASA, IRUWASA na DAWASA wakifanya kazi kubwa ya ujenzi wa miradi mikubwa kwa kutumia mapato yao ya ndani na ongezeko kubwa la mapato kwa kipindi cha miezi michache iliyopita tangu niwawekee malengo", ameongeza Profesa Mbarawa.

Akiwataka watendaji wote watakaopata nafasi RUWASA kufikia malengo na kuleta mabadiliko makubwa hususani vijijini ambao ni wahanga wakubwa wa tatizo la maji.

Wakati huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA), Profesa Faustine Bee akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa bodi za mamlaka za maji nchini amesema watafanya kazi kulingana na mikataba waliyosaini kwa lengo la kufikisha huduma ya maji ya uhakika.

Kikao hicho kimehusisha utiaji saini wa mikataba ya upimaji wa utendaji kazi wa mamlaka zote za maji kwa lengo la kuhakikisha zinatimiza majukumu yao kwa ufanisi.