Habari

Imewekwa: Jul, 23 2018

Wadau wa Sekta ya Maji Wakutana Kujadili Maendeleo ya Sekta ya Maji Nchini

News Images

Wadau wa Sekta ya Maji nchini wamekutana katika kongamano maalumu lililoandaliwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji lenye lengo la kujadili fursa zilizopo na changamoto zinazoikabili Sekta Binafsi nchini katika kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Sekta ya Maji nchini.

Kongamano hilo lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam ulishirikisha watendaji wakuu wa Idara za Serikali, Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umma, Washirika wa Maendeleo, Wakandarasi na Wawekezaji katika Sekta ya Maji ulilenga kuhamasisha wakandarasi wa ndani kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi ya maji na kuhamasisha matumizi ya vifaa vya ndani katika ujenzi wa miradi na utoaji wa huduma ya maji kwa ujumla. katika kutekeleza Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji nchini (WSDP II) kwa mafanikio.

Akifungua kongamano hilo aliyekuwa mgeni rasmi, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof. Makame Mbarawa, ametoa onyo kwa watendaji wote wa Sekta ya Maji kwa kuwataka wafanye kazi kwa weledi na kuacha ubabaishaji na kusema kuwa kwa muda mfupi aliokaa wizara hiyo amegundua miradi mingi inatekelezwa kwa uzembe, kutoa tenda kwa makandarasi wasiokuwa na uwezo, wasimamizi kutosimamia vizuri miradi na maandalizi duni ya miradi kutokana kuwa na uwezo mdogo ama kulipua kazi kwa baadhi ya watendaji.

Amesema katika WSDP I Serikali ililenga kuacha mwelekeo wake wa kuendesha miradi ya maji yenyewe kwa kushirikisha Sekta Binafsi. Programu hiyo iliyoanza Julai 2007 – 2016 kwa kushirikisha Sekta Binafsi katika kubuni, kupanga na kujenga miundombinu ya maji lakini haikufika lengo.

Pamoja na kugharimu kiasi cha Sh. tril 3.076, imeonyesha mapungufu kwa baadhi ya miradi kutokamilishwa; kujengwa lakini kutokuwa katika viwango vya ufanisi; ama kuchukua muda mrefu kukamilika.

Lengo kuu la WSDP II inayotekelezwa sasa ni kuwa na kasi ya utekelezaji wa miradi na kwa ufanisi unaokusudiwa, kadhalika kushirikisha Sekta Binafsi kwa ukaribu zaidi katika kubuni, kupanga kujenga (miundombinu) na kutoa huduma ya maji.

Matarajio yake ni kuwa kongamano hilo la siku mbili ni kuja na mapendekezo ya kuleta nguvu moja baina ya Serikali na Sekta Binafsi katika kufanikisha malengo ya Serikali katika kuleta maendeleo ya Sekta ya Maji nchini.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya, amehimiza wawekezaji, wafanyabiashara na wananchi kwa jumla kusoma Andiko la Serikali linalolenga kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Biashara na Uwekezaji. Ambapo Serikali kwa kushirikisha Sekta Binafsi imepitia sera, sheria, mifumo na miongozo inayosimamia Sekta ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji ili kubainisha kero na changamoto ambazo zinakusudiwa kuondolewa ili kufikia malengo ilijiwekea kama Serikali kwenye sekta hiyo.