Habari

Imewekwa: Oct, 11 2018

Tume ya Umwagiliaji Yahamishiwa Wizara ya Kilimo

News Images

Makatibu Wakuu wa Wizara za Maji na Kilimo wamekabidhiana nyaraka muhimu kuashiria kuhamishwa kwa Sekta ya Umwagiliaji kutoka Wizara ya Maji na Umwagilaji kwenda Wizara ya Kilimo.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara ya Maji, Dodoma kufuatia agizo la Serikali kuihamishia sekta hiyo Wizara ya Kilimo.

Lengo la kuihamisha Sekta ya Umwagiliaji ni kuongeza ufanisi katika matumizi ya umwagiliaji katika kilimo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo – awamu ya pili (ASDP II), na kuifanya Serikali kuchukua uamuzi wa kulihamishia jukumu la umwagiliaji kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwenda Wizara ya Kilimo.

Aidha, uamuzi huu umelenga kuiwezesha wizara yenye dhamana ya maji kudhibiti matumizi ya maji katika umwagiliaji bila kuwa na mgongano wa kimajukumu.

Sekta ya Umwagiliaji ndiyo inayoongoza kwa matumizi ya maji hapa nchini, yanayokadiriwa kufikia asilimia 83.6 ya matumizi ya maji yote nchini.

Kufuatia uamuzi huo wa Serikali, kwa sasa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itawajibika kiutawala kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo. Hivyo kufanya jina la Wizara ya Maji na Umwagiliaji sasa kuwa Wizara ya Maji.