Habari

Imewekwa: Oct, 27 2018

Tatizo la Maji Kisarawe Kuwa Historia

News Images

Wakazi wa Mji wa Kisarawe wanategemea kunufaika na Mradi wa Maji wa Kisarawe, utakaomaliza tatizo la muda mrefu la maji katika mji huo mkongwe.

Hii inatokana na Wizara ya Maji, kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es Salaam (DAWASA) kuanza ujenzi wa mradi huo mkubwa kwa lengo la kuwezesha Mji wa Kisarawe kupata maji ya kutosha kiasi cha lita milioni 4.08 kwa siku.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amempongeza Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa na Wizara ya Maji kwa utendaji mzuri na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji ili kuhakikisha huduma ya maji ya uhakika inapatikana kwa wananchi.

Ametoa pongezi hizo katika hafla ya uzinduzi wa utekelezaji wa mradi huo katika eneo la Mnarani, Kisarawe utakaochukua maji kutoka Ruvu Juu,
ambao utaigharimu Serikali Shingi Bilioni 10.85.

Amesema awali kulikuwa na tabia kwa miradi kusuasua, lakini sasa chini ya usimamizi wa Profesa Mbarawa miradi hiyo inaenda vizuri na huduma ya maji itaimarika.

Aidha, Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa amewahakikishia wakazi wa Kisarawe kero ya maji inayowakabili tangu mji huo uanze, kuwa ifikapo Julai, 2019 itabaki kuwa historia.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Maji Kisarawe, Profesa Mbarawa ameeleza unatekelezwa na mkandarasi CHICO kutoka China na utahusisha ulazaji wa bomba lenye urefu wa km 17 kutoka tenki la Kibamba mpaka Kisarawe mjini na ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita milioni 6 eneo la Mnarani, Kisarawe.

Amesema DAWASA itasimamia na kugharamia mradi huo kwa asilimia 100 , utakamilika ndani ya miezi 8.

Huku akizitaka mamlaka zote nchini, kufuata mfano wa DAWASA kwa kugharamia miradi yao wenyewe kwa fedha zao na kuiacha Serikali kugharamia miradi ya vijijini ambapo kuna changamoto kubwa ya maji.

Chimbuko la mradi huu agizo la Rais Magufuli la kutaka maji kutoka Ruvu Juu yafike katika mji wa Kisarawe wakati wa uzinduzi wa mradi wa upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Juu mnamo Juni, 2017.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Oktoba 27, 2018.