Habari

Imewekwa: Sep, 12 2018

Tanzania na Poland Zakutana Kujadili Jinsi ya Kuinua Sekta ya Maji Nchini

News Images

Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Ubalozi wa Poland nchini na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) imeandaa semina maalumu yenye lengo la kuanisha changamoto zinazoikumba Sekta ya Maji kwa nia ya kuzitatua na kuleta utekelezaji wenye tija na ufanisi kwa lengo la kuinua sekta hiyo nchini.

Semina hiyo ya siku mbili imelenga kupata uelewa wa pamoja wa changamoto zinazozikumba Sekta ya Maji; kuainisha maeneo muhimu kisekta yanayoweza kupata msaada kutoka Poland na OECD kulingana na ushirikiano uliopo baina ya washirika wa maendeleo na kujadiliana kuhusu sera sahihi ya utekelezaji wa makubaliano hayo katika maeneo yaliyoainishwa.

Akizungumza katika ufunguzi wa semina hiyo, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amesema ni mategemeo yake kuwa semina hiyo itasaidia kubadilishana uzoefu na kuainisha maeneo zaidi muhimu ya ushirikiano baina ya Tanzania, Poland na OECD.

Mhandisi Kemikimba amesema anategemea kuona maeneo ya ushirikiano yakilenga zaidi maendeleo na matumizi ya teknolojia bora katika kuongeza ufanisi kwenye matumizi ya maji na si kiholela kama ilivyo sasa kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania sasa na baadae.

‘‘Kwa kutumia uzoefu wa Poland tutakuwa na nafasi ya kukuza uchumi wetu kwa kuweka mifumo sahihi ya utunzaji, ukusanyaji na usambazaji wa maji ya kunywa; pamoja na mifumo bora ya umwagaji na kutibu majitaka. Pia, zifanyike tafiti sahihi kuhusu ubora wa maji; utambuzi wa vyanzo vya maji na teknolojia bora za umwagiliaji kwa lengo la kuinua kiwango cha uzalishaji katika kilimo na kuongeza usalama wa chakula nchini.’’, alisema Mhandisi Kemikimba.

‘‘Ni matumaini yangu kuwa msaada wa OECD katika kuboresha sera yetu ya maji, utakuwa chachu ya maendeleo na kufanikisha kufikia malengo tuliyojiwekea kisekta. Kikubwa ni OECD kuweka msukumo utakaoimarisha kiwango cha uwekezaji kwenye Sekta ya Maji; kuandaa na kutekeleza sera zitakazosaidia usimamizi bora wa maji zitakazochangia kuleta uchumi endelevu.’’, alisema Mhandisi Kemikimba.

Aidha, Mshauri Mwandamizi wa Sekretarieti ya Mahusiano ya Kimataifa wa OECD, Michael Laird amesema wataendelea kuangalia namna ya kuisaidia Tanzania hususani Sekta ya Maji na kupita semina hiyo wanategemea kujua maeneo watakayoweza kuisaidia Tanzania, kubadilishana uzoefu, kuimarisha uhusiano na kupanua wigo wa ushirikiano katika maeneo mengine zaidi.

Semina hiyo ni matokeo ya mkutano uliojadili ajenda iliyohusu maeneo ya ushirikiano kwa upande wa Sekta ya Maji baina ya Tanzania na Poland; kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo na Balozi wa Poland nchini, Krzyszfof Buzalski uliofanyika mnamo tarehe 29 Januari, 2018 katika ofisi za wizara hiyo jijini Dar es Salaam.