Habari

Imewekwa: Nov, 16 2018

Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi za Bonde la Mto Nile za Ukanda wa Maziwa Makuu

News Images

Tanzania itakua mwenyeji wa Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa nchi za Bonde la Mto Nile za Ukanda wa Maziwa Makuu -Nile Equatorial Lakes Council of Ministers Meeting (NELCOM).

Mgeni rasmi katika mkutano huu utakaofanyika jijini Dar es Salaam anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari ofisini kwake, jijini Dodoma, amesema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni; kupitia utekelezaji wa masuala mbalimbali ya miradi, kupokea taarifa ya utendaji, hali ya ulipaji wa michango ya kila mwaka kwa kila nchi mwanachama na tathmini ya watumishi wa Sekretariati ya Mipango -Nile Equatorial Lakes Subsidiary Action Program (NELSAP).

Amesema mkutano huo ni wa kiutendaji kwa kuwa Baraza la Mawaziri wa Maji ndio chombo cha juu kabisa cha maamuzi katika kusimamia na kuendesha shughuli za Bonde la Mto Nile katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Mkutano huu hufanyika mara moja kwa mwaka kwa kufuata mzunguko kwa nchi wanachama.

Profesa Mbarawa amesema ushirikiano huo una faida kubwa ambapo nchi zote wanachama zinafaidika na maji ya Mto Nile kwa kuwa na haki sawa ya matumizi ya maji, na kupitia ushirikiano huo Tanzania imefaidika katika maeneo mbalimbali ikiwamo mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo ambao unahusisha nchi tatu za Burundi, Rwanda na Tanzania, mradi huo upo katika hatua za ujenzi na unatarajiwa kuzalisha Megawati 80 ambazo zitagawanywa sawa kwa nchi hizo tatu.

Akifafanua zaidi kuhusu mkutano huo amesema Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Maji utatanguliwa na vikao vya wataalamu -Nile Equatorial Lakes Technical Advisory Committee (NEL-TAC) vitakavyoanza tarehe 20 hadi 21 Novemba, 2018 jijini Dar Es Salaam. Vikao hivyo vya wataalam ambavyo ni vya kiutendaji na hufanyika mara mbili kwa mwaka kwa kufuata mzunguko katika nchi wanachama.

Profesa Mbarawa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 za Bonde la Mto Nile zinazoshirikiana katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji za Bonde la mto huo, nchi nyingine ni; Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Misri, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan ya Kusini, Sudan, Uganda na Eritrea ambayo ni mtazamaji chini ya mwavuli na uratibu wa Nile Basin Initiative (NBI) yenye makao yake makuu Entebbe, Uganda

Aidha, amefafanua kuwa katika mkutano huo Tanzania ambayo ndio mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa nchiza Bonde la Mto Nile katika Ukanda wa Maziwa Makuu (NELSAP) itakabidhi uenyekiti kwa nchi ya Uganda.

Bonde la Mto Nile ni ukanda wote wa eneo la Bonde la Mto Nile kuanzia Ziwa Victoria hadi Bahari ya Mediterania, ambapo nchi yetu iko sehemu ya juu ya Bonde la Mto Nile ambako Mto Mara, Mto Simiyu na Mto Kagera inatiririsha maji katika Ziwa Victoria. Mto Nile ni miongoni mwa mito mirefu Duniani wenye kilomita 6,695 na ili kusimamia matumizi ya maji ya bonde la mto huo yenye usawa, nchi zote wanachama zinashirikiana.

Kitengo cha Mawasiliano

16 Novemba, 2018.