Habari

Imewekwa: Jan, 06 2019

TAARIFA KWA UMMA

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) leo ametembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa maji na jengo la Wizara ya Maji katika mji wa serikali eneo la Ihumwa Jijini Dodoma na kumsisitiza Mkandarasi kuzingatia muda katika ujenzi.

Waziri Mbarawa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi ya maji pamoja na ujenzi wa jengo la ofisi ya Wizara ya Maji na kuwahakikishia wakandarasi kulipwa fedha zao kwa wakati.

Waziri Mbarawa amesema mkandarasi wa mradi wa maji kampuni ya Oriental Construction Limited atalipwa fedha anazodai kwa kazi aliyoitekeleza, pamoja na hilo amezihakikishia Wizara na Taasisi zote zinazoendelea na ujenzi kuwa, kabla ya kumaliza ujenzi huduma ya majisafi na salama itakuwa imewafikia kikamilifu.

Akiwa katika eneo la ujenzi wa jengo la ofisiza Wizara ya Maji, Profesa Mbarawa alimtaka mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya SUMA JKT kufanya kazi kwa saa 24 kufidia siku zilizopotea awali katika utekelezaji wa kazi na kuzingatia mpango wa ujenzi kikamilifu. Aidha, ameagiza kupewa taarifa za maendeleo ya ujenzi kila siku.

Sanjari na hilo, Waziri Mbarawa ameielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Dodoma (DUWASA) kuweka mifumo ya usambazaji maji katika mji wa serikali kuanzia Jumatatu Tarehe 7 Januari, 2019 pia kuandaa mpango wa kuweka mifumo ya maji katika vijiji vilivyopo jirani na chanzo cha maji yatakayotumika kwenye mji wa serikali, chanzo hicho kinauwezo wa kuzalisha maji lita milioni mbili na nusu kwa siku. Pia ameagiza kupanda miti katika maeneo ya chanzo ili kiwe endelevu.

Kazi ya kufikisha majisafi na salama katika mji wa Serikali itakamilika ifikapo tarehe 20 Januari, 2019 na tenki la kupokea maji kutoka katika chanzo lenye uwezo wa lita za ujazo milioni moja liko katika hatua za mwisho za ujenzi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano

06 Januari, 2019