Habari

Imewekwa: Mar, 22 2019

Serikali Yakamilisha Zaidi ya Miradi ya Maji 1,595 Mijini na Vijijini

News Images

Serikali imefanikiwa kukamilisha miradi ya maji ipatayo 1,595 mijini na vijijini inayohudumia wananchi 25, 359, 290 sawa na asilimia 64.8 vijijini, wakati wananchi 11,563, 595 sawa na asilimia 85 waishio kwenye maeneo yanayohudumiwa na DAWASA, asilimia 80 kwenye miji mikuu ya mikoa na asilimia 64 kwenye miji mikuu ya wilaya, miji midogo na waishio kwenye maeneo yanayohudumiwa na Miradi ya Maji ya Kitaifa kwa upande wa mijini.

Mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji iliyo katika Awamu ya Pili katika komponenti zote zilizolengwa na programu hiyo ikiwemo kuinua kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa jamii na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa ametoa taarifa hiyo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 12 wa Pamoja wa Mapitio ya Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (Joint Water Sector Review) katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Gaspar Jijini, Dodoma huku akisema miradi mingine 500 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Ili tuweze kufikia malengo tuliyo nayo ya mwaka 2020, 2025 na 2030 wizara inafanya mabadiliko makubwa ili tuyafikie, tayari tuna Sheria Mpya ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2019 na tumeanzisha Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) yote haya yatatuwezesha kutoa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira nchi nzima kwa ufanisi.

Akitolea mfano Sera ya Maji ya Mwaka 2002 kuwa bado ina tija, lakini kutokana na mabadiliko mengi yametokea katika kipindi cha miaka 16 tangu ianze kutumika yakiwemo mabadiliko ya tabianchi, upatikanaji wa rasilimali za maji, teknolojia, na idadi ya watu. Kuna haja ya kuiangalia upya sera yetu ya maji, mikakati yake pamoja na kuandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Maji na Usafi wa Mazingira.

Profesa Mbarawa amesema mabadiliko mbalimbali yanaoendelea kwenye wizara na sekta kwa ujumla kimuundo, kimfumo na kiutendaji yamelenga kutoa ufumbuzi wa masuala mbalimbali ya maji kitaifa na kimataifa pamoja na kurahisisha utekelezaji wa miradi yote ya maji nchini.

‘‘Awamu ya pili ya proramu inaendelea vizuri, lakini bado tunahitaji fedha ili kuongeza kasi ya utekelezaji. Kati ya Shilingi bilioni 3.3 za kimarekani zinazohitajika, mpaka sasa tumeshapata Shilingi bilioni 1.9 za kimarekani huku Serikali ikiendelea kutafuta fedha zitakazofanikisha utekelezaji mzuri wa programu, amefafanua Profesa Mbarawa.

Hivyo basi, mategemeo yangu ni kuona mkusanyiko huu wa wataalamu unakuja na mawazo mapya yenye tija yatakayotoa ya changamoto zote za kiutekelezaji zinazotukabili na kutupa mwelekeo sahihi.

Vilevile, Profesa Mabarwa ameshukuru mchango mkubwa unaotolewa na Washirika wa Maendeleo katika kufanikisha maendeleo ya Sekta ya Maji Tanzania na kusisitiza wizara imelenga kukamilisha miradi inayoendelea kabla ya kuanza miradi mipya mijini na vijijini.

Wakati huo, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali itaendelea kuwathamini Washirika wa Maendeleo na wadau wote wa Sekta ya Maji kwa kuwa nao karibu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kupata faida ya uwekezaji mkubwa unaofanyika kwenye sekta.

Naye Mwakilishi wa Washirika wa Maendeleo, Lucas Kwezi amesema wanafurahishwa na mabadiliko yanayoendelea kwenye Sekta ya Maji na jambo hilo linatoa fursa kwao kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuinua kiwango cha upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira nchini.

Mkutano huo uliohusisha Serikali, Washirika wa Maendeleo na Wadau wa Sekta ya Maji umetoa fursa ya majadiliano ya kina kuhusu tathmini ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, pamoja na kuweka mikakati ya utekelezaji wa mpango kazi mahsusi kwa ajili ya mwaka ujao.