Habari

Imewekwa: Sep, 14 2018

Serikali Kuokoa Bilioni 2.9 Kutokana na DAWASA Mpya-Prof. Mkumbo

News Images

SERIKALI itaokoa Sh. bilioni 2.9 kila mwaka baada ya kuunganishwa kwa Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA).

Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo wakati wa hafla ya uzinduzi wa DAWASA mpya na kumtambulisha Afisa Mtendaji Mkuu mpya wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja. Hii ikifanyika mara baada ya kuunganishwa kwa mashirika ya DAWASA na DAWASCO pamoja

Prof. Mkumbo alisema Serikali ilikuwa ikipoteza fedha hizo katika uendeshaji wa mashirika hayo na baada ya muunganiko huo fedha hizo zitakwenda kusaidia upatikanaji wa huduma ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo ya Mkoa wa Pwani.

Amesema Serikali iliamua kuunganisha DAWASA na DAWASCO ili kupunguza matumizi na fedha, sasa hizi fedha zitatumika kuimarisha miundombinu na kuboresha huduma za maji katika maeneo yanayohudimiwa na DAWASA," alisema Prof. Mkumbo.

Prof. Mkumbo alionya wafanyakazi wa DAWASA mpya kuacha tabia ya dharau, kukumbatia matatizo na rushwa kwa wateja kwa kuwa Dar es Salaam inaongoza kwa malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu huduma isiyoridhisha.

‘‘Kulikuwa baadhi ya wafanyakazi wanadhani kutoa huduma ya maji kwa wananchi ni upendeleo na sio wajibu na haki, huku wengine wakiridhika na mafanikio madogo wakati wananchi wengi hawana huduma ya maji, na wengine wakiendekeza tabia ya rushwa’’, amesema Prof. Mkumbo.

‘‘Nataka Dawasa mpya kujiendesha kama kampuni binafsi inayolipwa na wananchi wa Dar es Salaam na Pwani na si wizara, ili kuongeza makusanyo ya fedha na waweze kujiendesha kwa faida’’, alisisitiza Prof. Mkumbo.

Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Luhemeja amesema wameweka malengo ya kukamilisha miradi mitatu na kutoa mwendelezo wa miradi mingine ndani ya siku 100.

Akiahidi ndani ya siku 100 watafunga mita mpya za malipo na kuhakikisha wanaanza ujenzi wa matenki ya maji Pugu na kukamilisha mradi wa visima vya Kimbiji na Mpera.