Habari

Imewekwa: Dec, 06 2018

Serikali Kumaliza Tatizo la Maji Oldonyosambu

News Images

Serikali imejipanga kumaliza tatizo la maji katika Kata ya Oldonyosambu iliyopo wilayani Arumeru katika mkoa wa Arusha kwa kuwaunganisha wakazi wa kata hiyo kwenye mradi mkubwa wa maji wa Jiji la Arusha.

Wakazi hao wa Oldonyosambu kwa muda mrefu wamekuwa na changamoto ya maji wanayotumia kuwa na kiwango cha madini ya fluoride, hivyo kusababisha athari kwenye mifupa, hususani meno.

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa amewataka wataalamu kutoka Mamlaka ya Maji jijini Arusha (AUWSA) kwenda kufanya usanifu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu itakayochukua maji kutoka mradi wa majisafi na usafi wa mazingira kwa Jiji la Arusha ambao umewekewa jiwe la msingi na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli utakaogharimu kiasi cha Sh. Bilioni 520 za kitanzania.

Amesema hakuna haja ya wananchi hao kuendelea kuathirika na matumizi ya maji hayo, wakati Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mradi huo wa Arusha mjini na inawezekana kufanyika utaratibu Oldonyosambu ikanufaika na mradi huo.

Profesa Mbarawa ameomba wakazi hao wawe wavumilivu, wakati wizara yake ikichukua hatua ya kukamilisha mpango huo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Arumeru, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amemshukuru Profesa Mbarawa kuchukua hatua hiyo na kulipatia ufumbuzi tatizo la maji na kuwataka wakazi hao kuendelea kuiamini Serikali yao kwa kuwa itaendelea kutatua kero zao kwa wakati.

Hatua ya Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa kufika katika Kata ya Oldonyo Sambu imetokana na agizo la Mhe. Rais Magufuli kumtaka waziri huyo kufika eneo hilo na kutafuta suluhisho ya kero ya maji kwa wananchi hao.