Habari

Imewekwa: Jan, 26 2019

Serikali kuhakikisha mradi wa maji wa Lendikinya-Monduli unakamilika

News Images

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkandarasi aliyepewa kandarasi ya mradi wa maji wa Lendikinya, pamoja na mhandisi wa maji wilayani Monduli wamekamatwa ili kutoa maelezo kuhusu mradi huo baada ya kuwa na kauli zinazokinzana kuhusu mradi huo wakati Serikali imeshatoa fedha kiasi cha shilingi milioni 521.7 ili wananchi wapate huduma ya maji safi.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema wizi na ubabaisha katika miradi ya maji unaumiza wananchi na hautavumilika kwa mhusika yoyote, awe ni mkandarasi au mtaalam wa serikali. Mkandarasi anayehusika katika mradi wa Lendikinya ni Jeremiak Z. Ayo Mkurugenzi wa kampuni ya Meero Ltd ya Arusha na mtaalam wa serikali wilayani Monduli Mhandisi Charles Masedoya.

Mradi wa maji wa Lendikinya ni kati ya miradi ya vijiji kumi inayotekelezwa wilayani Monduli kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP), na ulianza mwaka 2017, na miongoni mwa kazi za utekelezaji wa mradi ni pamoja na ulazaji wa mabomba kilomita 27, ujenzi wa vituo vya kuchota maji 12, ujenzi wa matenki mawili yenye uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo 90 na 135.

Ziara ya Naibu Waziri Aweso wilayani Monduli ilibainika kuwa miradi mingine ilishakamika isipokuwa mradi wa Lendikinya ambao hadisasa kazi zilizofanyika ni uchimbaji na ulazaji wa mabomba kilomita 23, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji tisa, ujenzi wa matenki mawili, pamoja na tenki la kupunguza msukumo (pressure), na mradi unatarajiwa kutoa huduma kwa wananchi elfu sita, pamoja na mifugo.

Utekelezaji wa miradi ya vijiji 10 kupitia programu ya sekta ya maji inatekelezwa na serikali pamoja na Benki ya Dunia.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano

26 Januari, 2019