Habari

Imewekwa: Sep, 12 2018

Profesa Mbarawa Aridhishwa na Kasi ya Utekelezaji ya Mradi wa Chalinze

News Images

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa maji Chalinze, ambao kwa muda mrefu umekuwa ukisuasua kitendo ambacho kimekuwa kero kubwa kwa waziri huyo.

Amesema hayo wakati alipokutana na Balozi wa India nchini, Sandeep Arya aliyefika ofisini kwake kwa mazungumzo ya maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya maji iliyo chini ya ufadhili wa Serikali ya India.

Profesa Mbarawa amemwambia Balozi Arya kuwa kwa sasa anaridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa Chalinze, tofauti na awali ambapo mradi huo umekuwa ukiongezewa muda wa kukamilika mara kwa mara kinyume na mkataba.

Akisisitiza kuwa kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo, anategemea utakamilika kwa wakati kulingana na makubaliano ya mkataba wa sasa na kuleta faraja kwa wakazi wa Chalinze na maeneo ya jirani, ambao kwa muda mrefu wamekua na kilio cha kukosa huduma ya uhakika ya majisafi na salama.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Arya amesema anafurahishwa na ripoti nzuri kuhusu mradi huo kwa kuwa nia ya Serikali ya India ni kuchangia maendeleo ya sekta hiyo nchini, lakini pia akataka kufahamu kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji wa Tabora, Igunga na Nzega hatua iliyofikiwa.

Aidha, Profesa Mbarawa amekubaliana na Balozi Arya kuwa kuna haja ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo kwenda nchini India kufanya mazungumzo na uongozi wa Benki ya Exim ya India kwa lengo la kuharakisha upatikanaji wa mkopo wa bei nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa huduma ya majisafi katika miji midogo 26 nchini.