Habari

Imewekwa: Dec, 06 2018

Profesa Mbarawa Amtaka Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Kuanza Ujenzi wa Mradi wa Bonyokwa Mara Moja

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa amemtaka Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja kuanza kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Bonyokwa Jumatatu, Desemba 10 na kumaliza tatizo la muda mrefu la maji katika Kata ya Bonyokwa.

Amesema hayo leo wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Bonyokwa wakati akiwa ziarani Tabata mkoa wa kikazi wa DAWASA kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

"Najua viongozi wengi wamefika Bonyokwa na mmepewa ahadi nyingi, lakini mimi ndiye msimamizi mkuu wa Sekta ya Maji nawahakikishia tutakeleza mradi huu na ni lazima ukamilike", amesema Profesa Mbarawa.

"Nataka Mhandisi Luhemeja uwepo hapa Jumatatu na kazi ianze , kama ni suala la vibali nitalifuatilia mimi mwenyewe vitapatikana mpaka kufikia mwishoni mwa wiki ili kazi ianze mara moja", ameagiza Profesa Mbarawa.

Amesema hakuna sababu ya Jiji la Dar es Salaam kukosa maji ya uhakika, ikizingatiwa ni jiji kuu la biashara nchini. Hivyo, ni lazima maeneo yote ya jiji hilo yawe na huduma ya maji ya uhakika.

Wakati huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Lujemeja amesema tayari baadhi ya vifaa vimeshafika na kusisitiza wataanza kazi rasmi Jumatatu.

Bonyokwa ni moja ya maeneo yaliyowekewa mkakati mkubwa wa kufikisha huduma ya majisafi na salama kutokana na kuwa moja ya maeneo yenye tatizo kubwa la maji kwa Jiji la Dar es Salaam.