Habari

Imewekwa: Sep, 12 2018

Profesa Mbarawa Akutana na Balozi wa Ufaransa Kujadili Ujenzi wa Bwawa la Farkwa

News Images

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier kwenye Makao Makuu ya Wizara, jijini Dodoma kujadili ujenzi wa Bwawa la Farkwa.

Profesa Mbarawa amefanya mazungumzo hayo na Balozi Clavier aliyeambatana na baadhi ya Maseneta kutoka katika Bunge la Juu la Ufaransa, kwa lengo la kupata ufadhili kutoka Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa Bwawa la Farkwa ambalo linategemea kuongeza upatikanaji wa maji katika jiji la Dodoma, ambalo chanzo chake kikuu cha maji ni visima virefu ambavyo havikidhi mahitaji ya wakazi wa jiji hilo.

Profesa Mbarawa alimshukuru Balozi Clavier kwa kufika ofisini kwake pamoja na Serikali ya Ufaransa kwa ujumla kupitia Shirika lake la Maendeleo la (AFD) katika kufadhili utekelezaji wa miradi ya maji nchini na sekta hiyo kwa ujumla.

Vilevile, Profesa Mbarawa alimuomba Balozi Clavier ufadhili katika kufanikisha ujenzi wa Bwawa la Farkwa, ambalo Serikali ya Tanzania imeshaanza hatua za kutafuta fedha kwa wadau wengine kufanikisha mpango huo.

‘‘Ujenzi wa bwawa hili ni muhimu ikizingatiwa, jiji la Dodoma ndio makao makuu ya nchi na Serikali hivyo ni lazima tuchukue hatua mahsusi ili kuhakikisha huduma ya maji inaimarika kwa kuwa kutakuwa na taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi, viwanda na ongezeko kubwa la watu. Hivyo bwawa hili ni moja ya hatua ya kuwa na huduma ya uhakika kwenye makao makuu ya nchi, tunaomba mtusaidie jambo hili’’, alisema Profesa Mbarawa.

Wakati huo, Balozi Clavier alisema Ufaransa itaendelea kuwa mdau mkubwa maendeleo wa Tanzania na itachukua hatua ili kufanikisha mpango huo na utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji nchini.

Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Dodoma (DUWASA inatarajia kutekeleza mradi wa Bwawa la Farkwa katika Wilaya ya Chemba. Bwawa hilo litazalisha maji kiasi cha lita 120,000,000 kwa lengo la kufikisha huduma kwa watu milioni moja kwenye mji wa Serikali na maeneo mengine ya jiji la Dodoma.