Habari

Imewekwa: Oct, 06 2018

Profesa Mbarawa Aipongeza Amcow kwa Kazi Nzuri

News Images

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Nchi za Afrika (AMCOW) ametoa pongezi nyingi kwa Mtendaji Mkuu wa AMCOW, Dkt. Canisius Kanangire na Sekretarieti ya AMCOW kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuinua Sekta ya Maji na Usafi wa Mazingira barani Afrika pamoja na changamoto nyingi walizonazo.

Profesa Mbarawa ametoa pongezi hizo katika mazungumzo kati yake na Dkt. Kanangire aliyemtembelea ofisini kwake Dodoma kwa lengo la kumpa taarifa ya utekelezaji ya baraza hilo kwa miaka miwili na maandalizi ya Mkutano ujao wa Baraza la Mawaziri utakaofanyika Libreville, Gabon mwishoni mwa mwezi huu.

Profesa Mbarawa amesema anatambua changamoto za kifedha, kiutumishi na uendeshaji za AMCOW, lakini amemshukuru Dkt. Kanangire na kuipongeza Sekretarieti yake kwa utendaji wao mzuri na kumuahidi ushirikiano wa kutosha kutoka kwake kama Mwenyekiti na Tanzania kama mwananchama wa baraza hilo.

Aidha, Dkt. Kanangire ameipongeza Tanzania kwa kazi kubwa waliyoifanya tangu ichukue Uenyekiti wa AMCOW mwaka 2016 na anajivunia Afrika Mashariki kutoa uongozi makini uliotoa mchango mkubwa uliochangia kuinua Sekta ya Maji na Usafi wa Mazingira kwa kuhakikisha ubora na usalama wa maji kwa bara la Afrika na upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi wake.

Tanzania inategemea kumaliza muda wake wa uenyekiti wa baraza hilo baada ya miaka miwili kama katiba inavyosema na kukabidhi kwa nchi ya Gabon, lakini itachukua Uenyekiti wa Mfuko wa Maji wa Afrika (African Water Facility) kwa miaka miwili ijayo kuanzia 2018-2020 kutoka kwa nchi ya Senegal.