Habari

Imewekwa: Oct, 11 2018

Profesa Mbarawa Aahidi Ushirikiano kwa DDCA na Chuo cha Maji

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa ameahidi kuzipa ushirikiano taasisi za Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) na Chuo cha Maji (Water Institute) na kuzihakikishia kuwa wizara itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha zinatimiza majukumu yake ya msingi.

Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo leo wakati alipozitembelea taasisi hizo zilizo chini ya Wizara ya Maji kwa dhumuni la kuzungumza na watumishi wake ili kuweza kujua changamoto zao kiutendaji na namna ya kuzisaidia ili ziweze kufanikisha malengo yake.

Akiwa DDCA Profesa Mbarawa ameitaka taasisi hiyo kujipanga vizuri kwa kuweka mikakati mizuri ya kibiashara ili kuendana na mahitaji, na kufikia malengo ya kutoa huduma bora ya ujenzi wa mabwawa na uchimbaji visima ndani na nje ya nchi.

Amesema anataka kuiona DDCA ikiwa na uwezo wa kujiendesha vizuri yenye mashine na vitendea kazi vya kutosha kwa kuwa ndio msingi wa utendaji kazi wao na mafanikio yao katika shughuli wanazozifanya.

‘‘Ninataka kuona mkichimba visima 700 kutoka 400 kwa mwaka na mkitoa huduma bora na yenye viwango kwa hilo sina mashaka kutokana na uzoefu na kazi ambazo mmekwishazifanya, naamini uwezo huo mnao na mtafikia malengo hayo’’, alisema Profesa Mbarawa.

‘‘Wizara itafanya kila liwezalo kufanikisha majukumu yenu ya msingi, pamoja na kuwalipa fedha zenu kikubwa ni kujituma na kuwa na mikakati mizuri na endelevu, kwa hilo tutawapa ushirikiano wa kutosha’’, aliongeza Profesa Mbarawa.

Vilevile, Profesa Mbarawa ameahidi kutumia wataalamu wanaozalishwa na Chuo cha Maji kwa lengo kuinua maendeleo ya Sekta ya Maji nchini kwa kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kutumia wataalamu wake wa ndani katika kufanikisha utekelezaji wa miradi yake ya maji.

Amesema hayo huku amekitaka chuo hicho kuwaandaa wataalamu wenye uwezo na uadilifu ambao watakuwa na uzalendo watapokuwa wakilitumikia taifa, ili kuondokana na matumizi ya wataalamu kutoka nje ambao baadhi yao wamekuwa wakikosa uzalendo na kutokujali maslahi mapana ya taifa.

‘‘Tumeshaanza utaratibu wa kuchukua wataalamu kutoka katika Chuo cha Maji na vyuo vingine nchini, kwa mfano DAWASA wamechukua mafundi sanifu 100 na kuwaajiri. Rai yangu kwenu ni kuhakikisha mnaadaa wataalamu wenye uwezo na maadili ili waweze kuwa manufaa kwa taifa sasa na baadae’’, alisisitiza Profesa Mbarawa.

Huku akiahidi wizara itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kusomesha wataalamu na kukisaidia chuo kuweza kudumu gharama za uendeshaji na kukijengea uwezo zaidi wa kudahili wanafunzi wengi zaidi na kutoa elimu bora.

Imetolewa na

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Maji.