Habari

Imewekwa: Dec, 06 2018

Profesa Mbarawa Aagiza Wakazi wa Salasala Waunganishiwe Huduma ya Maji

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASA) kuwaunganishia huduma ya maji wakazi wa Salasala ili waanze kupata majisafi na salama, na kuondokana na adha ya matumizi ya maji yasiyokuwa salama.

Profesa Mbarawa ametoa maagizo hayo leo wakati alipokuwa akiendelea na ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi wa Jiji la Dar es Salaam, baada ya wananchi wengi kuonekana wakihitaji kufanyiwa maunganisho kwenye Mradi wa Maji wa Salasala kutokana na kutokana na gharama kubwa wanazotumia kununua maji kutoka kwa watu binafsi.

Akiwa Salasala Profesa Mbarawa amemuagiza Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja kuleta mafundi wasiopungua hamsini (50) waje kufanya kazi ya maunganisho kwa wateja wote wanaohitaji kuunganishwa kwenye mtandao na kuongeza wapya ambao wameonekana ni wengi.

Nataka waje mafundi wa kutosha kuanzia kesho ili kazi ya kuwaunganisha wateja wapya iende kwa kasi kubwa, hakuna sababu ya wananchi hawa kuendelea kutumia gharama kubwa kupata maji wakati kuna mtandao wa maji kutoka Ruvu Chini wenye maji ya uhakika na uwezo wa kufanya kazi hiyo mnao.

Nimuonye Meneja wa Maji Tegeta nataka zoezi hili likamilike, vinginevyo nitakaporudi tena na kukuta bado nitachukua hatua. Niombe wananchi mtoe ushirikiano katika jambo hili na mnipe taarifa kuhusu zoezi hili.

Vilevile, Profesa Mabarawa amemuagiza Meneja wa Miradi DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi kuhakikisha kazi ya kufukia mitaro ya mabomba inakamilika mara moja na wananchi waanze kupata maji.

Aidha, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amefika Kinzudi, Kata ya Goba kufuatilia upatikanaji wa huduma ya maji baada ya kukamilika kwa ulazaji wa mabomba mapya wa maji Kinzudi, ambapo amekuta maji yameanza kutoka katika eneo la Kwa Mtenga.

Mradi wa Maji wa Salasala unategemea kunufaisha wakazi 40,000 wa Salasala ikiwa ni mikakati ya Serikali kumaliza tatizo la maji kwa maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam.