Habari

Imewekwa: Jul, 16 2018

Prof. Mbarawa Awataka Wakandarasi Kumaliza Mradi Haraka

News Images

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mh. Prof. Makame Mbarawa amewataka wakandarasi wanaotekeleza mradi wa maji wa Nzega, Igunga na Tabora kukamilisha kazi hiyo kwa haraka na kwa ubora wa hali ya juu kama ilivyo kwenye mkataba.

Mhe. Prof. Mbarawa alitoa maelekezo hayo alipotembelea mradi huo eneo la Igunga na Nzega kujionea ubora wa kazi na hatua ya mradi ulipofikia.

Akisoma taarifa ya hali yamaji ya Halmashauri ya Igunga, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo alisema changamoto kubwa kwa sasa kwa Malaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga (IGUWASA) ni madeni makubwa wanayodaiwa na wakandarasi pamoja na maji yanayopotea.

Alipokuwa akiongea na watumishi wa halmashauri na wataalamu wa maji wa Igunga Prof. Mbarawa amekerwa na tabia za mamlaka za maji kushindwa kudhibiti maji yanayopotea.

“Kila unapokwenda unaambiwa asilimia 40 ya maji yanapotea, hili halikubaliki kabisa, najua sababu za maji kupotea ni hitilafu katika dira za maji, uvujaji kwenye mabomba chakavu na kubwa zaidi ni wizi wa maji ambao ndiyo sababu kubwa, kwani ingekuwa maji yanavuja tungeyaona barabarani”. Alisema Profesa Mbarawa.

Aidha, amezitaka mamlaka zote za maji nchini kuhakikisha wanakuja na mkakati wa kuzuia maji yanayopotea, kwa kubaini wezi wa maji na kuwashughulikia watumishi wasio waadilifu wanaoshirikiana na wezi wa maji.