Habari

Imewekwa: Jul, 05 2018

Mh. Prof. Mbarawa Ampa Mkandarasi Miezi Mitatu Kukamilisha Mradi wa Maji

News Images

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mh. Prof. Makame Mbarawa amempa miezi mitatu mkandarasi kutoka Kampuni ya Jain ya India inayotekeleza mradi wa uboreshaji wa mfumo wa usambazaji maji jijini Dar es Salaam unaosimamiwa na DAWASA, kukamilisha mradi huo ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba.

Hii imetokana na mara baada ya Mh. Prof. Mbarawa kutembelea baadhi ya maeneo ya mradi huo na kutokuta mafundi wala kazi yoyote ikiendelea, huku mkandarasi huyo akishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kutokana na hali hiyo.

Mh. Prof. Mbarawa amemuonya mkandarasi huyo endapo atashindwa kukamilisha mradi huo kwa wakati, atafutiwa usajili katika Bodi ya Wakandarasi na hatafanya tena kazi nchini kwa kuwa Serikali haitavumilia tabia ya utekelezaji mbovu wa miradi yake ya maji.

‘‘Nimepita baadhi ya maeneo sijakuta chochote kinachoendelea, sikubaliani na jambo hili.Kwa sababu kama ni fedha mkandarasi ameshalipwa zote mpaka hatua aliyofikia, lakini bado mradi unasuasua. Naagiza mpaka kufikia mwisho wa mwezi Septemba mradi huu uwe umekamilika kama mkataba unavyosema, vinginevyo tutafuta usajili wake kwenye Bodi ya Wakandarasi na itakuwa kazi yake ya mwisho kufanya Tanzania’’, alisema Mh. Prof. Mbarawa.

Aliendelea kusema kuwa ni lazima mradi huo ukamilike ili wananchi waanze kupata maji, ambapo unategemea kuhudumia wakazi 300,000 wa maeneo ya Salasala, Bunju, Wazo, Changanyikeni, Bagamoyo, Kibamba, Kiluvya, Mbezi Luis na mengineyo. Ikiwa ni hatua ya kutimiza lengo la kufikia wateja 850,000 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja alilowapa DAWASCO.

Vilevile, Mh. Prof. Mbarawa amesema kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi mingi ambayo Serikali imepanga kuitekeleza ili kuhakikisha wakazi wa Dar es Salaam na maeneo ya Pwani wanapata maji ya uhakika ifikapo mwaka 2020.