Habari

Imewekwa: Jul, 06 2018

Prof. Mbarawa Aitisha Kikao cha Dharura Kupata Ufumbuzi wa Mradi Chalinze

News Images

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof. Makame Mbarawa ameitisha kikao cha dharura ili kupata ufumbuzi wa utekelezaji wa mradi wa maji wa Chalinze, ambao kwa muda mrefu umekua ukisuasua na kusababisha kutokamilika kwa wakati.

Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za wizara zilizopo Dar es Salaam na kuhusisha DAWASA (wasimamizi wa mradi), Overseas Infrastructure Alliance Pvt Ltd (Mkandarasi), Shanxi Construction Engineering Group Corporation ya China (Mkandarasi-mshiriki) na WAPCOS Ltd ya India (Mtaalamu Mshauri) kwa lengo la kupatia ufumbuzi unaosababisha kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo.

Prof. Mbarawa ameitisha kikao hicho mara baada ya kumaliza ziara yake aliyoifanya ya kukagua maendeleo ya mradi wa maji wa awamu ya tatu ya upanuzi wa chanzo na mtandao wa maji wa Chalinze unaotekelezwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji na kusimamiwa na DAWASA na kutoridhishwa na uwezo wa mkandarasi anayetekeleza mradi.

Katika ziara hiyo Prof. Mbarawa alitembelea na kujionea kazi za upanuzi wa chanzo, ujenzi wa matenki, ulazaji wa mabomba, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji, pamoja na ujenzi wa ofisi mpya za uendeshaji wa mradi huo.

Hata hivyo, amekerwa na kasi ya utekelezaji ya mkandarasi ambaye ameonekana kuwa na uwezo mdogo wa kufanya kazi hiyo kutokana na kusababisha mradi huo uliokuwa ukamilike tangu Februari, 2017 kuongezwa muda mara kwa mara bila mafaniko.

‘‘Nimegundua mkandarasi ndiye chanzo cha kusuasua kwa mradi huu. Kwa kuwa kama ni pesa sio tatizo, zimekuwa zikitolewa lakini utendaji wake bado umezorota. Kwa kifupi, uwezo wa mkandarasi ni mdogo’’, alisema Prof. Mbarawa.

‘‘Mimi niliyepewa dhamana ya kusimamia sekta hii nampa muda mpaka kufikia mwezi Novemba na sio mwezi Disemba tena kama mkataba wake unavyosema, awe amekamilisha mradi huu. Vinginevyo, tutamchukulia hatua kwa kumfutia usajili na utakuwa mwisho wake kufanya kazi nchini na wala asisumbuke kuomba kazi nyingine yoyote kwa kuwa hatopata tena’’, alisisitiza Prof. Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa ameishukuru DAWASA na pamoja viongozi waliopita kwa juhudi zao za kuhakikisha mradi huo unatekelezwa vizuri na kwa wakati na kusema kuwa mradi huo kwa sasa ni lazima ukamilike ili wakazi wa maeneo ya Chalinze, Bagamoyo, Ngorongoro na Handeni waweze kupata maji.

Naye, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Dkt. Sufiani Masasi amesema watahakikisha wanasimamia maagizo ya waziri na kuchukua hatua stahiki ili mradi uweze kukamilika kwa ajili ya maendeleo ya Chalinze na maeneo ya jirani.