Habari

Imewekwa: Dec, 06 2018

Nataka Bohari Kuu Isambaze Dawa za Kutibu Maji-Profesa Mbarawa

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa amesema anataka kuona Bohari Kuu ya Maji (Maji Central Stores) inasaidia katika kupunguza gharama za madawa ya kutibu maji nchini na kusambaza vifaa mbalimbali kwenye Mamlaka za Maji nchini.

Ameyasema hayo alipotembelea taasisi hiyo iliyo na ofisi zake Boko, jijini Dar es Salaam na kutoridhishwa na utendaji na uongozi wa taasisi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Profesa Mbarawa amesema nia ya Serikali ni kuona mamlaka zinafaidika na Bohari Kuu ya Maji kwa kusambaza vifaa vyake kwa Mamlaka za Maji nchini.

Profesa Mbarawa amesema, kuna mita zaidi ya 10,000 zimefungiwa tu ndani baadala ya kutumika kwenye mamlaka mbalimbali, pia kuna miradi mingi imesimama kutokana na kukosa vifaa, wakati Bohari Kuu ya Maji imeviweka na havifanyi kazi yoyote.

Amemtaka Boharia Mkuu wa taasisi hiyo, Crepin Bulamu ndani ya wiki mbili awe amesambaza mita hizo kwa mamlaka za maji nchini, ikiwemo Mamlaka ya Maji mjini Lindi (LUWASA) ambayo ina uhitaji wa mita za maji 3,000 maeneo mengine pia.

"Hii ni mara yangu ya kwanza kufika hapa kwa lengo la kufahamu na kujifunza namna taasisi hii inavyofanya kazi. Lakini nimekuta vifaa vingi sana ambavyo vinahitajika kwenye miradi inayoendelea na mingine imesimama kwa kukosa vifaa bila kutumika, hii inaonyesha utendaji wa watu hawa hauko makini na hauniridhishi", amesema Profesa Mbarawa.

"Nataka kuona Bohari Kuu ni inajipanga upya na kuanza kuuza dawa za kutibu maji kwa mamlaka na wao watakuwa wakinunua kutoka kutoka kiwandani moja kwa moja na sio kwa watu au kampuni binafsi", amesisitiza Profesa Mbarawa.

Naye Boharia Mkuu, Crepin Bulamu amesema, ni kweli wana vifaa vingi ila vyenye ubora ila ataanza kusambaza vifaa hivyo kwa mamlaka za maji nchini kulingana na maelekezo ya waziri.

Huku akiagizwa kuteketeza dawa zote zilizoisha muda wake zisije kwenda kwa mamlaka kwa ajili ya matumizi na kuleta athari kwa binadamu.