Habari

Imewekwa: Jan, 08 2019

NAIBU WAZIRI WA MAJI AMCHUKULIA HATUA MHANDISI WA MAJI SHINYANGA KWA KUSHINDWA KUKAMILISHA MRADI KWA WAKATI

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesikitishwa na Mradi wa Maji wa Mwakitolyo kutotoa maji licha ya Serikali kuwa imeshatoa asilimia 98 ya fedha zote kwa ajili ya utekelezaji wake.

Hali iliyosababisha Naibu Waziri Aweso kuliagiza Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kumkamata Mhandisi wa Maji Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Sylivester Mpemba kwa kushindwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo utakaoigharimu Serikali Shilingi bilioni 1.482.

Amechukua hatua hiyo wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Mwakitolyo, kwenye mkutano wa hadhara ambapo hakuridhishwa na maendeleo ya mradi huo, licha ya awali kutaka mradi huo uwe umekamilika mwezi Aprili, 2018 wakati wa ziara yake aliyoifanya Disemba, 2017 mkoani Shinyanga.

Naibu Waziri Aweso alishangazwa na kitendo cha Serikali kulipa Shilingi bilioni 1.462 kwa Mkandarasi Halem Construction Co. Ltd na mradi ukiwa bado hautoi huduma kwa wananchi, huku taarifa ikionyesha kuwa una tatizo litakalohitaji kufanyiwa usanifu upya.

Hali iliyomfanya kutaka kujua kilichosababisha hali hiyo wakati awali walisema tatizo ni fedha na zikatolewa, na kutoridhishwa na majibu yaliyotolewa na Mhandisi Mpemba.

“Mradi wa Maji Mwakitolyo gharama yake ni Shilingi bilioni 1.482 mpaka sasa Serikali ya imeshalipa Shilingi bilioni 1.462, kiasi kilichobaki ni Shilingi milioni 20 tu na wananchi bado hawana maji na Serikali inalaumiwa kwa sababu ya uzembe wa watendaji, niseme hili halikubaliki", alisema Aweso.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa atatuma mara moja timu ya wataalamu kutoka wizarani, alipokuwa akiongea nae mbele ya mkutano huo kwa njia ya simu alipotaka kujua ni lini atatuma wataalamu kwa lengo la kupata ufumbuzi wa tatizo la mradi huo haraka.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Solwa, Ahmed Salum ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo na ana uhakika tatizo la maji Mwakitolyo linaenda kuisha.