Habari

Imewekwa: Dec, 14 2018

Naibu Waziri Aweso aanza Ziara ya Kikazi Lindi

News Images

Naibu wa Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso ameanza ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maji katika mkoa wa Lindi kwa kutembelea Miradi ya Ng’apa, Kimeng’ene na Chikonji na kuagiza hatua zichukuliwe kurekebisha kasoro zote za miradi na kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.

Naibu Waziri Aweso amewataka wasimamizi wa Sekta ya Maji mkoani Lindi kuongeza nguvu ya utekelezaji wa miradi yote inayoendelea ili ikamilike, kwa kuwa hali ya upatikanaji wa maji Lindi hairidhishi wakati akipokea taarifa ya huduma ya maji iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa aliyekuwa safarini.

Akiwa kwenye Mradi wa Maji Ng’apa unaohudumia Manispaa ya Lindi, Aweso ameihakikishia Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Lindi Mjini (LUWASA) kuwa atasimamia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuongeza mtandao kwa maeneo ambayo hayana mtandao kwa kiasi cha kilomita 40 kama ilivyo kwenye bajeti ya 2018/19.

Huku akiwataka watendaji wa LUWASA wahakikishe wanajipanga kwa kutumia vizuri mapato ya ndani ili kuongeza mtandao wa maji ili waongeze wateja, watakaochangia ongezeko la mapato kwa mamlaka hiyo.

Pia, ameiagiza Wizara ya Maji kufanya marekebisho ya pampu mbili za kusukuma maji mara moja, mara baada ya pampu hizo ambayo ni miongoni mwa pampu tatu kuharibika na kubaki pampu moja tu. Jambo linalohatarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa mji wa Lindi, endapo pampu iliyobaki ikipata tatizo mji huo utakosa maji kabisa.

Akiongea na wakazi wa Kijiji cha Kimeng’ene kwenye mkutano wa hadhara alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza ahadi zake kwa vitendo na imedhamiria Kumtua Mama Ndoo ya Maji Kichwani kwa kumsogezea huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza karibu na makazi yao.

Katika mradi wa Kimeng’ene unaotumia nishati ya dizeli, Aweso alilazimika kuongea na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kuweza kupata umeme wa REA kwenye mradi huo. Ili mradi huo uanze kutumia nishati ya umeme ukizingatia ni umbali wa kilimomita 2 tu kutoka kwenye nguzo za umeme hadi kwenye mradi. Jambo ambalo wananchi watatakiwa kuchanga asilimia 18 ya gharama za kupeleka umeme kwenye mradi kiasi ambacho wameshachangia.