Habari

Imewekwa: Feb, 11 2019

‚ÄčNaibu Waziri Aweso Aipongeza IRUWASA kwa Kazi Nzuri

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso ameipongeza Mamlaka ya Maji ya mjini Iringa (IRUWASA) kwa kazi nzuri inayofanya katika kutoa huduma ya majisafi kwa manispaa ya mji wa Iringa kwa asilimia 96.

Naibu Waziri Aweso ametoa pongezi hizo wakati alipokua akizungumza na watumishi wa mamlaka hiyo mara baada ya kujionea miradi inayotekelezwa na mamlaka hiyo wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi katika manispaa ya mji wa Iringa leo.

''IRUWASA ni moja ya mamlaka tunazojivunia kama wizara kutokana na kazi yenu nzuri na mimi binafsi nimejionea jambo hili kwa kufika hapa, hii inatokana na uongozi mzuri wa Mkuregenzi Mtendaji na Bodi yenu, pamoja na watumishi mlio nao'', amesema Aweso.

''Mmepiga hatua kubwa kiteknolojia kwa matumizi ya mita za kulipia kabla ya matumizi (prepaid meters, kukusanya madeni kutoka kwa wateja waliokuwa wadaiwa sugu, teknolojia ya ukusanyaji mapato na kuwaunganishia wateja wapya huduma miongoni kazi nzuri mnazozifanya'', amesema Aweso.

Aidha, Naibu Waziri Aweso ameitaka mamlaka hiyo kuongeza nguvu katika ujenzi wa mfumo wa majitaka ambao umefikia asilimia 40 na kufikisha huduma ya maji ya uhakika katika eneo la Nduli kwa kushirikiana na manispaa kwa kuwa bado huduma hiyo ni changamoto kwa wakazi wa eneo hilo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa IRUWASA, Gilbert Kayange amesema mpaka sasa wameweza kufunga prepaid meters 1857 tangu mwaka 2016 na kupunguza madeni kwa taasisi za Serikali kwa asilimia 30.

Kayange ameongeza kuwa wameweza kupunguza tatizo la upotevu wa maji mpaka kufikia asilimia 24.5 na wamejipanga kufanikisha zoezi la kupeleka maji katika eneo la Nduli kwa lengo la kufikisha asilimia 100 ya huduma ya maji kwa manispaa hiyo.

IRUWASA imekuwa ni mamlaka ya mfano kwa upande wa matumizi ya prepaid meters kwa mafanikio na immekuwa ni sehemu ya mamlaka nyingine za maji nchini katika kujifunza kuhusiana na matumizi ya mita hizo.