Habari

Imewekwa: Jul, 23 2018

Naibu Waziri Aweso Afunga Kongamano la Wadau wa Sekta ya Maji

News Images

Wadau wa Sekta ya Maji zaidi ya 200 wamehitimisha kongamano la siku mbili na kuazimia kujenga mazingira yatakayoleta mwelekeo mpya wa kufanikisha Sekta ya Maji nchini haraka iwezekanavyo, kwa Serikali kupanua wigo wa kuihusisha Sekta Binafsi nchini huku wakiongozwa na Sera ya Taifa Maji ya mwaka 2002 na Mpango wa Awamu ya Pili wa Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II).

Kongamano hilo lililoandaliwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji lililowahusisha Wakandarasi, Wataalamu Washauri, Wawekezaji na Wadau wa Maendeleo nchini lililenga kuinua kiwango cha uhusiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi nchini chini ya wenyeviti wenza Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya.

Kabla ya kuweka saini ya makubaliano ya azimio lililofikiwa wakati wa kufunga kongamano hilo, washiriki waliangalia maeneo kadhaa ya kujenga uhusiano baina ya Serikali na Sekta Binafsi, na kubaini changamoto kadhaa zikiwemo kuimarisha menejimenti ya ugavi serikalini. Pia, kuhakikisha manunuzi kutoka viwanda vilivyopo nchini vinapewa kipaumbele na kukutana mara kwa mara ili kuwa na mawasiliano ya karibu katika ngazi zote katika sekta. Azimio hilo linasisitiza uzalendo wa kuona umuhimu wa kuliendeleza Taifa.

Katika makubaliano hayo, yamo masuala ya kuimarisha mahusiano na wadau wa maendeleo katika meneo ya teknolojia na rasimali hususani kwenye majisafi na majitaka. Vilevile, kamati maalumu imeandaliwa kwa ajili ya kuandaa mwendelezo wa andiko la utekelezaji wa dhamira ya Serikali, ambayo ni kuongeza wigo wa wa ushirikiano wa Sekta Binafsi katika nyanja zote kama moja ya agenda muhimu katika Andiko la WSDP II.

Aidha, Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata majisafi, salama na yenye kutosheleza bila kufikiria gharama, wakati mfanyabiashara unawaza faida. Kuna haja ya sote tuwe na uzalendo wa kitaifa kwa jamii yetu.

‘‘Ili kufanikisha mahusiano ya Sekta Binafsi na Serikali ni lazima sekta zote zijenge tabia ya kupeana taarifa sahihi kuhusu kila jambo. Mtaalam u mshauri anapoandaa pendekezo la mradi asifanye maamuzi ya ushauri holela ya kuwa bidhaa zinazozalishwa nchini hazifai, kwa kuwa manunuzi ni muhimu yaanzie toka viwanda vyetu na wawekezaji nchini wapewe kipaumbele na wizara italisimamia hilo ili wawekezaji wa ndani wawe na uhakika wa masoko.

Akifunga kongamano hilo Naibu wake Jumaa Aweso, amesisitiza kuna umuhimu kwa kila kundi katika sekta kwa maana ya wakandarasi, wataalamu washauri, wagavi na menejimenti za ufundi kutambua umuhimu wa kutimiza wajibu kwa weledi ili kila jambo linalopangwa litimie pasipo kukwama, huku akisisitiza kila mradi unaoanzishwa, uandaliwe kwa ufanisi na usikwame kwa visingizio vya makosa ya nyuma na ukamilike kwa wakati.