Habari

Imewekwa: Jan, 15 2019

Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018 wawasilishwa kwa kamati

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Wizara ya Maji imewasilisha Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018 (The Water Supply and Sanitation Bill, 2018) kwa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji.

Lengo la muswada ni kutungwa kwa Sheria mpya ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2019 ambayo itasimamia utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira nchini.Aidha, inapendekezwa kufutwa kwa Sheria za Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira, Sura 272 na Sheria ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam, Sura 273, ili kuwa na sheria moja itakayosimamia kikamilifu shughuli zote za utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira katika ngazi mbalimbali nchini.

Muswada huu unamadhumuni ya kuwa na sheria madhubuti itakayosimamia masuala ya utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira nchini.Aidha, Sheria inayokusudiwa itaweka vyombo mbalimbali vya usimamizi wa utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira katika ngazi mbalimbali ili kuhakikisha usimamizi bora, ufanisi na uendelevu katika utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira nchini. Mambo muhimu yatakayozingatiwa katika muswada ni yafuatayo;

Kubainisha majukumu ya watendaji au wasimamizi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na majukumu ya Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa, majukumu ya Sekretarieti ya Mkoa, na majukumu ya Mamlaka za Serikali za Mitaa;

Kuanzishwa kwa Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira (Water Supply and Sanitation Authorities), ambazo zitaanzishwa na Waziri wa Maji kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa;

Kuainishwa kwa majukumu ya Mamlaka za Maji;

Uteuzi wa Bodi za Mamlaka za Maji na masharti ya uteuzi wa watoa huduma;

Kueleza majukumu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (The Energy and Water Utilities Regulatory Authority-EWURA);

Ushiriki wa jamii kwa kuanzisha vyombo vya watumiaji maji (Community Based Water Supply Organizations) na kuainisha masharti mbalimbali yanayohusu uanzishwaji na umiliki wa pamoja yakiwemo masuala ya fedha;

Kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini (Rural Water Agency – RUWA) ambao utasimamia miradi na utoaji wa huduma ya maji vijijini, ikiwemo uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa;

Kuainisha majukumu ya RUWA na uongozi wake ambao utasimamiwa na Bodi itakayoanzishwa kwa mujibu wa Sheria hii;

kuendelea kutambuliwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Taifa wa Maji (National Water Fund).Lengo la Mfuko huu ni kutafuta fedha kwa ajili ya kusaidia uwekezaji katika miradi ya maji;

Kuweka makosa na adhabu chini ya Sheria hii, masharti ya ujumla na masharti ya mpito.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano

15 Januari, 2019.